Na JANETH MUSHI
-ARUSHA
MANUSURA Wilson Tarimo wa ajali ya basi la shule ya Lucky
Vincent lililoua wanafunzi 32, walimu wawili na dereva anatarajiwa kupanda
kizimbani kutoa ushahidi upande wa Jamhuri dhidi ya kesi inayomkabili mmiliki
wa shule hiyo Innocent Moshi.
Mwanafunzi Tarimo aliyekimbizwa nchini Marekani kwa matibabu
zaidi yeye na wanafunzi wenzake wawili, atakuwa miongoni mwa mashahidi 15 wa
Jamhuri katika kesi namba 78 ya Mwaka huu.
Mtuhumiwa Moshi pamoja na Mwalimu Mkuu Msaidizi Longino Nkana
walisomewa hoja za awali jana katika Mahakama ya wilaya ya Arumeru mkoani hapa.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo,Desderi
Kamugisha, Wakili wa Jamhuri Khalili Nuda,alisema kuwa Jamhuri wanatarajia kuwa
na mashahidi 15 katika kesi hiyo pamoja na vielelezo 12.
Mashahidi wengine ni Afisa Kazi Mfawidhi wa Idara ya Kazi Mkoa
wa Arusha,Wilfred Mdemi,Mohamed Matumula kutoka Kampuni ya Bima ya Zanzibar
Insurance,Songoyi Jilala(Askari wa usalama barabarani Arusha),Koplo Hamad
(Karatu),Inspekta Shukrani (Askari wa usalama barabarani Arusha),Komplo
Saada(Traffic Arusha) na E.4312 PC Mugobe Traffic Arusha.
Wengine ni Mkuu wa Polisi wa Usalama barabarani Mkoa wa
Arusha(RTO),Nuru Suleiman,G 4130 PC Mwita(Askari wa usalama barabari
Karatu),Ignatus Paul(Karatu),Leonidas Gerald(Morombo) na Hamis Omary mkazi wa
Sombetini.
Wakili Nuda alitaja vielelezo hivyo kuwa ni kadi ya gari lenye
namba za usajili T 871 BYS,mkataba wa ununuzi wa gari,Barua ya RTO kwenda
Sumatra ya Mei 8 mwaka huu,barua ya RTO kwenda Zanzibar Insurance ya Mei 8
mwaka huu,taarifa ya Zanzibar Insurance ya Mei 9 mwaka huu.
Vingine ni taarifa ya Sumatra ya Mei 9 mwaka huu,taarifa ya
idara ya kazi,taarifa ya ukaguzi wa gari,ramani ya eneo la tukio,maelezo ya
mshitakiwa wa kwanza na maelezo ya mshitakiwa wa pili,ambapo wakili huyo
aliiomba mahakama hiyo kutoa ya wito kwa mashahidi hao.
Akiwasomea hoja hizo za awali,Wakili Nuda alidai mahakamani hapo
kuwa katika kosa la kwanza linalomkabili Moshi,ni kufanya biashara ya
usafirishaji abiria bila kuwa na leseni ambapo kati ya Desemba 12 mwaka jana
hadi Mei 6 mwaka huu,alitumia gari katika barabara ya umma aina ya
Mitsubishi Rossa T. 871 BYS,kubeba wanafunzi.
Alidai kuwa kosa la pili ni kuruhusu gari hilo kutumika bila
kuwa na bima kati ya kipindi cha Desemba 16 mwaka jana na Mei 6 mwaka huu.
Kosa la tatu ni kushindwa kuingia mkataba na mwajiriwa wake kati
ya Juni Mosi mwaka jana hadi Mei 6, Mwaka huu akiwa mmiliki wa gari hilo
alishindwa kuingia mkataba wa ajira kinyume na sheria za ajira na dereva wako
Dismas Gasper ambaye kwa sasa ni marehemu.
Katika kosa la nne,Mushi anadaiwa kubeba na kuzidisha
abiria 13 ambapo Mei 6, mwaka huu akiwa Mmiliki wa Kampuni ya Lucky
Vincent,katika maeneo ya Kwa Morombo,aliruhusu garinuilo kubeba abiria 38
badala ya abiria 25.
Katika kesi hiyo Nkama anakabiliwa na shitaka moja ambalo ni
kuzidisha abiria katika chombo cha usafiri ambapo akiwa muandaaji wa
safari hiyo ya wanafunzi aliruhusu abiria zaidi ya 13 kupanda katika gari hilo
ambalo lilipaswa kuwa na abiria 25.
"Baada ya tukio uchunguzi ulifanyika katika mamlaka za
kutoa leseni ikiwemo Sumatra na Kampuni ya Bima ya Zanzibar Insurance na zote
zilionyesha gari halikuwa na kibali cha kufanya biashara ya kubeba wanafunzi
wala bima halali kwa mujibu wa sheria,"alidai
Baada ya kusomewa maelezo hayo Moshi alikiri gari hilo kwenda
Karatu likiwa halina bima huku Mwalimu Mkuu Msaidizi akikiri mahakamani hapo
kuwa alizidisha abiria katika safari hiyo.
Awali kabla ya kuwasomea maelezo ya awali,Wakili huyo aliiomba
mahakama kuifanyia marekebisho hati hiyo ya mashitaka.
Hakimu Kamugisha aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 28 mwaka
huu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ambapo mashahidi hao wa upande wa
jamhuri wataanza kutoa ushahidi ambapo pia aliwataka mawakili wa pande zote
mbili kuhakikisha wanakuwepo mahakamani kwani siku hiyo hatapanga kusikiliza
kesi nyingine zaidi ya hiyo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment