HIFADHI ya Taifa ya Ruaha inayopakana na vijiji 64 vilivyopo
katika mikoa minne imefanikiwa kudhibiti matukio ya mioto vichaa inayohatarisha
maisha ya viumbe hai na kambi za watalii ndani ya hifadhi hiyo.
Matukio ya kuwapo kwa mioto vichaa yalitajwa kusababishwa
na majangiri au wananchi wanaoishi maeneo jirani na hifadhi hiyo wakati wanapokuwa
wana andaa mashamba yao kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Akitoa ufafanuzi kudhibitiwa kwa mioto hiyo kwenye kipindi
cha Hifadhi za Taifa, “Uhifadhi endelevu kwa maendeleo” kinachoandaliwa na
Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), kupitia Kituo cha Televisheni ya Taifa
(TBC), Muikolojia Msaidizi Daniel Mathayo alisema, mbinu hizo zimesaidia
kukabili tatizo hilo.
Daniel alizitaja mbinu hizo kuwa ni hifadhi hiyo kuwasha
mioto ya awali katika maeneo hatarishi ili kuzuia mioto vichaa inayoweza
kuwashwa baadaye na kusababisha uharibifu mkubwa ndani ya hifadhi.
“Kazi hii ya kuwasha moto wa awali hufanyika kila mwaka
baada ya mvua kukatika ambapo huwa tunafanya kabla ya majani hayajakauka
kutokana na kuzibabua nyasi ili tusimalize kabisa chakula cha wanyama,” alisema
Daniel na kuongeza:
“Kitendo hiki ni muhimu sana kwasababu kiangazi kinapoanza
kukaribia husaidia kuzuia mioto vichaa inayoweza kusababishwa na majangiri, au
jamii inapoandaa mashamba, sasa tusipofanya moto wa awali unapokuja moto kichaa
unaweza kusababisha madhara zaidi hifadhini,” alisema.
Danieli alizitaja faida muhimu nyingine za kuwashwa kwa
moto wa awali kuwa ni pamoja na kusaidia kukuza majani au chakula cha wanyama
pori kwani kunapokuwa na majani yaliyokaa miaka mingi bila kuwapo majani mapya
si afya kwa wanyama na viumbe hai wengine.
“Unapokuwa na mlundikano wa kila mwaka wa majani ndani ya
hifadhi kwa hakika si vizuri kwa wanyama kwa moto wa awali pia hutusaidia
kuleta chakula kipya kwa wanyama. Lakini pia husaidia shughuli za kitalii kwani
ukichoma baadhi ya maeneo watalii wanapokuwa hifadhini huwaona wanyama kwa
urahidi,” alisema Daniel na kuongeza:
“Jambo jingine moto wa awali huwasaidia askari wa hifadhi
kufanya doria na ulinzi kwa wanyama kwa usalama zaidi kutokana na sehemu nyingine
kutoonekana vizuri na kupitika kirahisi kwa magari au miguu ili kuwaona
majangiri,” alisema .
Akielezea historia ya Hifadhi ya Ruaha ambayo ndio hifadhi
kubwa zaidi nchini ikiwa na Kilometa za mraba 20,226, Mkuu wa Hifadhi hiyo
Christopher Timbuka alisema, Ruaha inapatikana katika mikoa minne ambayo ni
Mbeya, Njombe, Dodoma wilayani Chamwino na sehemu kubwa ya Hifadhi ikipatikana
mkoani Iringa.
“Ufikaji katika hifadhi unaweza kutumia njia kubwa mbili
ambazo ni kutokea Iringa kwa barabara mpaka Ruaha na kutoka wilayani Mbarari
mkoani Mbeya. Jitihada zinaendelea za kuongeza njia nyingine mbalimbali ikiwazo
za kutokea Chunya mpaka Mbeya, Igurusi mpaka kuingia hifadhini,” alisema
Timbuka.
Makala hizo za utalii kumewezesha wananachi kuendelea kuzijua
zaidi Hifadhi za Arusha, Tarangire yenye Tembo wakubwa, Hifadhi ya Kilimanjaro
yenye Mlima mrefu kuliko yote Afrika, Hifadhi ya Mkomazi yenye Swala Twiga,
Serengeti, Lubondo, Hifadhi ya Udzungwa, Kitulo na Hifadhi ya Manyara iliyopo
yenye Simba wapandao miti.
No comments:
Post a Comment