Wednesday, August 9, 2017

EWURA YATAKIWA KUDHIBITI VIBALI VYA LESENI



MAMLAKA ya udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura),imetakiwa kudhibiti utoaji wa vibali vya leseni kwa watoa huduma wakiwemo wa vituo vya mafuta,wasiokidhi masharti na taratibu zilizowekwa ikiwemo matumizi ya  mashine za kielekrtoniki (EFD's). 

Agizo hilo lilitolewa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Mrisho Gambo,wakati alipokuwa akizindua ofisi za Ewura  Kanda ya Kaskazini,itakayohudumia mikoa ya Arusha,Tanga,Kilimanjaro na Manyara.

Alisema kuwa watoa huduma wasiotambua wajibu wao kwa kutumia mashine hizo,wanaisababishia hasara serikali hivyo Ewura kama wasimamizi wana wajibu wa kuhakikisha kuwa wanasimamia kudhibiti mapato ya serikali yasipotee hivyo wasitoe vibali kwa mtu ambaye hajakidhi vigezo.

"Ewura hakikisheni mnapotoa leseni kwa mtu anayefungua kituo cha mafuta,sharti ka kwanza awe na amshine ya kielektroniki ili serikali iweze kupata mapato na kupeleka huduma kwenye maeneo mengine.Watu wenye taasisi wenyewe wanatakiwa wasimamie mambo yao,wasisubiri mpaka viongozi wa kiasiasa wakimbizane na masuala ambayo kimsingi mtaalamu alitakiwa ashughulike nayo,"alisema na kuongeza

"Watanzania wamekuwa na tabia ya kupuuza maagizo ya serikali,wakati wa usimamizi  unapofika ndiyo maneneo mengi yanakuja,ni vizuri kuanzia mwanzoni,msisubiri mtu afungue kituo cha mafuta halafu baadaye muanze kukimbizana naye,"

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka hiyo,Profesa Jamidu Katima,alisema ofisi hiyo ya Kanda ni ya pili kufunguliwa hapa nchini,ambapo ya kwanza ipo mkoani Mwanza.

Alisema kuwa lengo la ofisi hizo za Kanda ni  kusaidia kusogeza huduma na kutatua changamoto zinazowakumba watoa huduma na wananchi ambapo pia wanatarajia kufungua ofisi nyingine katika Nyanda za Juu Kusini itakayokuwa mkoani Mbeya na Kanda ya Kati,Dodoma.


No comments:

Post a Comment