Thursday, July 20, 2017

UTANGULIZWE UZALENDO BARABARA YA SAKINA –TENGERU

KUBORESHWA na kujengwa upya kwa miundombinu ya barabara hususani kwa Jiji la Arusha linalopatikana Kaskazini mwa Tanzania kumezidi kuongeza muonekano na mvuto zaidi kwa wageni na wenyeji.

Kwa miaka mingi jiji hilo limefananishwa au kuitwa ‘Geneva ya Afrika” kutokana na mambo mengine ikiwamo hali ya hewa ya baridi huku wadau wengine nao wakilibariza kuwa Jiji la wapendanao.

Jiji la Arusha limekuwa kitovu kikuu katika sekta ya utalii nchini, biashara ya madini ya vito ya Tanzanite.Lakini pia utalii wa mikutano japo kwa sasa umedorora ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Kuwapo kwa Makao Mkuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), inayojumuisha nchi wanachama Kenya, Tanzania, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudani Kusini kumeendelea kulifanya jiji hilo kuwa la kipekee zaidi nchini.

Kilimo cha vitunguu eneo la Mang’ola wilayani Karatu nacho kimekuwa na mchango mkubwa katika kuliendeleza jiji hilo kwani zao hilo limekuwa likichangamkiwa zaidi na wafabiashara kutoka nchini Kenya.

Lakini kwa upande wa shughuli za ufugaji Jiji hilo halipo nyuma sana kutokana na kuzungukwa na Halmashauri za wilaya zinazojishughulisha na ufugaji na hivyo kuwafanya wakazi wake kuwa walaji wazuri wa nyama choma.

Yote hayo na mengine ambayo sijayaainisha katika makala yangu kwa umoja wake yameendelea kukuza kipato cha mti mmoja mmoja na hata jiji kwa ujumla wake.

Si nia yangu kujielekeza katika shughuli za kijamii na uchumi zinazowaingia kipato wakazi wa Jiji la Arusha na maeneo jirani, bali nakusudia kuwekana sawa katika umuhimu wa kuitumia vizuri miundomboni ya barabara mpya kujiletea maendeleo.

Naandika mtazamo huu huku nikiwa natambua kwamba tayari kwa asilimia 90 barabara mpya na ya kisasa kabisa inayoanzia eneo la Sakina jijini Arusha hadi Tengeru wilayani Arumeru ikiwa inaelekea ukingoni kukamilika.

Ukiutazama kwa jicho la kawaida, lazima utabaini ujenzi huo umetumia gharama kubwa sana mpaka utakapo kamilika ukiwa ni sehemu ya ujenzi wa barabara za Afrika Mashariki kuelekea Holili mkoani Kilimanjaro mpaka upande wa Kenya.

Barabara hizi zimeondoa kabisa msogamano wa magari ulioanza kujitokeza kwa watumiaji wa barabara ya Moshi- Arusha hasa wanapoingia jijini Arusha au maeneo Mianzini, Sakina, Ngaramtoni kuelekea Namanga mpakani mwa Kenya.

Hivyo basi kutokana na kukamilika kwa barabara hizo na zinazoendelea kujengwa ipo haja kwa watumiaji wa barabara wote kuzitunza ili ziweze kuhudumia kizazi cha sasa na kijacho kwani haitakuwa na maana kuanza kuharibu miundimbinu iliyopo kwa muda mfupi tangu iwekwe.

Nimelazimika kuyasema haya kwa kutambua wazi kwamba tayari baadhi ya watumiaji wa barabara hizi za Sakina mpaka Tengeru wameanza kuonyesha ukosefu wa uzalendo wa kupenda na kutadhamini vitu vyao.

Wapo baadhi ya madereva wasio waungwana ambao tayari wameanza kuvunja baadhi ya kingo zinazojengwa pembezoni mwa barabara kutokana tu na kutokuwa makini katika uendeshaji wa vyombo vyao vya moto.

Nitumia fursa hii kutahadharisha madereva kusukumwa zaidi na uzalendo wa kutunza miundombinu ya barabara hizo hasa kingo zilizowekwa kwenye madaraja pamoja na maeneo yenye miiunuko.

Watanzania tunafahamiana asije kutokea kati yetu akasukumwa na tamaa ya kufungua kingo na kwenda kuziuza vyuma chakavu hakika atakuwa ametenda unyama kwa wananchi zaidi ya Milioni 120 wa Afrika Mashariki.

Achilia mbali uvunjwaji wa kingo hizo za alminiam zipo pia Taa za barabarani ambazo nazo zimewekwa kwa gharama, sitegemei baada ya kuanza kutumika kutokee uharibifu usio wa lazima kama kugongwa na madereva walevi au wazembe.

Kupitia Mtazamo huu nitoe tahadhari kwa jeshi la polisi mkoani Arusha hususani askari wa Usalama barabara kuanza kutumia muda mwingi katika barabara hiyo ili kukamata madereva wote wanaokiuka sheria.

Mpaka naandika mtazamo huu wapo baadhi ya madereva wa magari, pikipiki kuendelea kuendesha vyombo vyao kwa mazoea na kujikuta wakisababisha ajali zisizo za lazima.

Mfano katika ujenzi huo kumetengwa michepuko ya kuingia, kutoka na kugeuza gari lako. Lakini baadhi ya madereva wameendelea kulazimisha kupita upande wa barabara usio sahihi kwao na kujikuta wakihatarisha usalama barabara.

Kama hilo halitoshi barabara za pembeni zilizotengezwa hususani kwa basi ya abiria kushusha na kupakia sasa yamegeuzwa kuwa maegesho ya magari ya wateja wa Bar, Bodaboda na vitu vingine.

Kupitia mtazamo huu niwaombe askari wa usalama barabarani kuongeza kasi ya kufanya ukaguzi lakini pia kwa mamlaka zinazohusika kuwakamata na kuwatoza faini madereva wote wanaogesha magari yao kinyume cha sheria za usalama barabarani.

Mwisho.


No comments:

Post a Comment