Na RASHIDI NCHIMBI
-JESHI LA POLISI ARUSHA
WAKUU wa Vituo vituo vidogo,
Wakaguzi wa Tarafa na Polisi Kata wametakiwa kuwa karibu na wananchi hasa kwa
kushiriki shughuli za kijamii kama vile misiba na matatizo mbalimbali hatua
iakayowasaialia wao kupata taarifa nyingi za uhalifu.
Akizungumza katika kikao kilichohusisha
watendaji wa kata mbalimbali za halmashauri ya Jiji la Arusha mwishoni mwa wiki
mjini hapa Kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha Charles Mkumbo alisema, kutatua
matatizo ya kihalifu yanayowakabili wananchi si njia pekee ya kuwa karibu na
wananchi bali askari wanatakiwa kushiriki kwa namna moja shughuli za kijamii
katika maeneo yao.
Alisema kitendo hicho cha askari
hao kuishi vizuri na wananchi nje ya kazi yao ya Upolisi kitasabaisha wananchi
wajione wapo karibu na askari kwa kila jambo hali ambayo itasaidia kupata
taarifa zaidi za kihalifu ambazo hatimaye watazifanyia kazi.
”Ushirikiano wenu pia ujikite
kushiriki katika masuala ya kijamii kama vile misiba, lakini pia kuna matatizo
mengine kama ya kukatika kwa umeme Polisi Kata unapaswa uwasiliane na TANESCO
ili kujua tatizo lipo wapi na kisha kuwajulisha wananchi wa kata yako,”alisema
Kamanda Mkumbo.
Aidha Kamanda Mkumbo alisisitiza
kudumishwa kwa ushirikiano baina ya askari na viongozi wa mitaa pamoja na kata
ili kujenga umoja imara utakaosaidia kupambana na uhalifu na kuwaeleza
watendaji nao wanatakiwa kuwaambia mabalozi wawe na madaftari la usajili wa
wageni katika maeneo yao yatayowawezesha kujua tarehe ya kuingia na kuondoka
hali ambayo itasaidia kuimarisha usalama.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa
Kata ya Ngarenaro Brayson Nassari aliendelea kuhimiza ushirikiano katika
utendaji wa kazi baina ya Polisi kata na watendaji hali ambayo itasaidia
kuimarisha utulivu na amani ndani ya jiji la Arusha.
Naye Mkuu wa Polisi wilaya ya
Arusha Emmanuel Tille aliwasisitiza Polisi kata kuwa na vikao vya mara kwa mara
na wananchi hali itakayowasaidia kutoa elimu ya ulinzi shirikishi na kupata
taarifa lakini pia aliwaeleza watendaji wa kata waendelee kutoa taarifa na
kufichua sehemu zenye viashiria vya uhalifu ili zifanyiwe kazi kwa haraka.
Kuwapo kwa mahusiano ya karibu
baina ya Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha na wananchi kumesaidia kwa kiasi
kikubwa kupunguza vitendo vya uhalifu ambapo takwimu za hivi karibu
zilizotolewa na Kamanda Mkumbo zinaonyesha kwa kipindi cha miezi 6 tangu Januari hadi Juni Mwaka huu uhalifu umepungua kwa asilimia 24.4 ikilinganishwa na kipindi
kama hiki Mwaka 2016.
No comments:
Post a Comment