KAULI ya Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi kwamba kama si matakwa
ya Katiba ya nchi, uongozi wa Rais John Magufuli ulipaswa kuendelea kuwapo
miaka yote, imeendelea kupingwa vikali na wadau nchini.
Akizungumza na MTANZANIA jana mjini hapa aliyewahi kuwa Naibu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Serikali ya awamu ya Nne, Dk.
Goodluck Ole Medeye aliwataka viongozi wastaafu wasiwatamanishe raia kubadili
Katiba ya nchi.
Akifafanua hatari ya kauli iliyoanza kuenea miongoni mwa baadhi
ya wananchi alisema, hatua hiyo ni mbaya kwani inaweza kuleta kiongozi asiye na
maadili (fisadi) na mwisho wa siku wananchi wakashindwa kumtoa.
“Niwashauri viongozi wetu hususani wastaafu wasitutamanishe
kubadili Katiba kwa sababu ya utendaji wa kiongozi aliyepo madarakani, hii ni
hatari sana,” alisema Dk. Medeye na kuongeza:
“Maoni ya Mzee Mwinyi ni mazuri tunaya heshimu. Hata hivyo ni
vizuri kutambua kuwa Katiba hiyo ambayo yeye alishiriki kuitunga iliweka ukomo
wa utumishi kwa nafasi ya Rais.
“Ili kuendeleza amani tulio nayo kwani nina amini umeiona
matukio kwenye nchi za Kiarabu. Lakini kwetu sisi Tanzania imetusaidia kuibua
vipaji bora zaidi katika uongozi.
“Kama Katiba isingeweka ukomo na hivyo kwa kuzingatia uhodari wa
Rais Jakaya Kikwete leo hii tungempataje Rais Dk. Magufuli?” Alihoji.
Dk. Medeye aliyewahi pia kuwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru
Magharibi kabla ya kukimbilia Chadema kisha UDP aliwataka wananchi kote nchini
kumuunga mkono Rais Dk. Magufuli kwa kazi anazoendelea kulifanyia taifa.
“Niwaombe Watanzania tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu ambariki
rais aliyepo kwa sasa ili atuongoze vema katika kipindi cha uongozi wake,”
alisema Dk. Medeye.
Akitoa salamu za Eid El Firti katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Dar
es Salaam Mzee Mwinyi alinukuliwa na vyombo vya habari akisema laiti ingelikuwa
Katiba iliyopo haikufupisha muda wa uongozi wa rais angeshauri Rais Magufuli
awe rais wa Tanzania siku zote.
Alisema mambo anayoyafanya Rais Magufuli ni mazuri na
yanalipeleka taifa mbele, kwani ameweza kufanya mambo mengi kwa kipindi kifupi
kuliko yaliyowahi kufanywa na watangulizi wake akiwamo yeye (Mwinyi).
“Nchi imetulia, leo mnakwenda madukani hospitali ofisini unapata
huduma nzuri. Hayo ndio tuyliyoyataka, kupata serikali itakayokuwa na watumishi
ambao watawatumikia watu na hivyo ndivyo inavyofanya ssa kwa sababu tumepata
kiongozi tuliyenaye leo” alisema Mzee Mwinyi na kuongeza:
“Huyu kiongozi ni wa kumuenzi sana, ni wa kumsaidia sana ni wa
kumsifu sana, si kumsifu kwa uongo, uongo ni kumsifu kwa kazi nzuri anayoifanya
si kwa manufaa yake bali kwa manufaa ya Watanzania wote pamoja na mimi
niliyesimama hapa,” alisema.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment