Na MWANDISHUI WETU
-MANYARA
WANANCHI wanaopakana na eneo huru la kibiashara
la uwekezaji (EPZ), katika Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro, mkoani
Manyara wameiomba Serikali kubainisha mpaka unaowatenganisha na eneo hilo.
Wakazi hao wamedai kuwa mpaka halali wa
eneo la EPZ ni hekta 510.64 na si hekta 530.87 kama zinavyobainishwa kwani
mpaka uliokuwapo awali unaonyesha hivyo pamoja na vibao vilivyopo sasa.
Wakizungumza jana katika eneo la
Mirerani, wananchi hao walidia kuwa walifikisha kilio chao kwa Waziri Mkuu
Kasimu Majaliwa alipofanya ziara yake mkoani Manyara, Februari Mwaka huu alipofika
Mirerani.
Akizungumza kero hiyo Mchungaji Michael
Mtero alisema Waziri Mkuu Majaliwa alimuagaiza Mkuu wa Mkoa huo Dk. Joel
Bendera kufuatilia mgogoro huo na kuupatia ufumbuzi hivyo wanahitaji kujua
hatima ya suala hilo.
“Mimi nilipatiwa eneo hili ili nijenge
kanisa na muumini mmoja ambaye alijitolea sadaka kiwanja chake ila naambiwa
kuwa sehemu ya uwanja ipo katika mpango wa EPZ,” alisema mchungaji
Mtero.
Blasto Mosses alisema alijenga nyumba
baada ya kuuziwa eneo hilo na kupata nyaraka halali kutoka serikalini lakini
anashangazwa kuambiwa kuwa nyumba na kiwanja kipo ndani ya sehemu ya EPZ.
Israel Loserian alisema hivi sasa
wameshikwa na sintofahamu ya tatizo hilo kwani ni muda mferu walikuwa
wanamiliki maeneo yao na hivi karibuni kuambiwa kuwa wapo ndani ya uwekezaji wa
EPZ.
Michael Lekopito (95) alisema alizaliwa
kwenye eneo hilo lakini anashangazwa kuambiwa kuwa wamevamia sehemu hiyo ambayo
hawakulipwa fidia yao kama baadhi ya watu walivyolipwa.
Hata hivyo, mkuu wa wilaya hiyo mhandisi
Zephania Chaula alisema waliopo kwenye eneo hilo wapo kimakosa kwani mpaka
unaonyesha kuwa wameingia ndani ya na walishawaambia waondoke wenyewe.
Mhandisi Chaula alisema walishawaeleza
waliouziwa sehemu hiyo wabomoe, kwani awali serikali ilileta mpimaji wakagoma,
wakamleta mpima wao akasema wapo ndani ya eneo, hata fedha hawakumlipa.
“Hivi sasa Wizara ya Nishati na Madini
inatarajia kujenga jengo lao kubwa la madini house kwenye eneo hilo na pia
tunatarajia kuweka mtaro ili kubainisha vizuri mpaka wa EPZ,” alisema Mhandisi
Chaula.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment