Friday, June 2, 2017

WADAU WA UTALII ARUSHA WAWEKA MIKAKATI


Na MWANDISHI WETU
-ARUSHA 

WADAU wa Utalii mkoani Arusha wamekutana kujadili mikakati ya kuipaisha sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi.

Majadiliano hayo yalifanyika mjini Arusha juzi, na kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo, Chama cha Wafanyabiashara wa Utalii (TATO) na Shirika la Hifadhi za Taifa nchini (TANAPA).
Akizungumza katika warsha hiyo Gambo alisema mkoa wa Arusha umekuwa ukichangia mapato ya utalii nchini kwa zaidi ya asilimia 80. Hivyo kuna kila sababu ya kuboresha sekta hiyo ili iendelee kuleta matokeo chanya kwa taifa.
Gambo katika mkutano huo aliwataka wadau hao kushirikiana na viongozi wa mkoa kuandaa tamasha kubwa la utalii la kimataifa litakalotumika kama jukwaa la kuutangaza mkoa na taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Allan Kijazi akizungumzia kuhusu tozo kuwa kubwa alisema bado kuna muda wa kuendelea kujadili jambo hilo.
“Tunaamini awamu ya tano ni sikivu, ni vyema tukipanga muda sisi wadau tujadiliane tuone namna ya kuishauri Wizara,” alisema Kijazi.
Aidha, TATO katika mkutano huo waliainisha changamoto wanazokutana nazo katika biashara hiyo.
MWISHO. 

No comments:

Post a Comment