Monday, June 19, 2017

WALIOSHINDWA KULIPA KODI YA ARDHI KUTAIFISHWA MALI ZAO

WANANCHI  80  waliofikishwa Mahakama ya   Ardhi Mkoa wa Arusha, kwa kushindwa kulipa kodi ya ardhi, wameanza  kutaifishiwa mali zao kutokana na kukiuka ulipaji wa kodi za serikali, ambazo zimefikia Sh.Bilioni 2.2.


Akizungumza mwishoni mwa wiki mara baada ya kuwasilisha hati za madai 40 kati ya 80,Kaimu Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Kanda ya Kaskazini, Leo Komba  alisema wameamua kuwafikisha wadaiwa hao mahakamani, ili madalali wapige mnada mali zao kutokana na kukaidi kulipa kodi ya ardhi.

“Hawa watu tumegawa makundi awamu mbili, hivyo awamu hii 40 watalipa Sh.bilioni 1.1 na awamu ya pili watawasilisha hati zingine za watu 40 atakaolipa Sh.bilioni 1.1,”alisema.
Alisema wameamua kuchukua hatua hiyo, baada ya kutoa matangazo na kukaa kwa muda wa miezi miwili bila kulipwa fedha za serikali wanazodaiwa, ila kutokana na ukaidi wao ndio maana wameamua kufika Baraza la Ardhi ili mahakama ichukue hatua.

Komba alisema zoezi la kudai fedha hizo lililianza mapema mwezi Aprili mwaka huu na walisambaza hati za madai 3500 kwakushirikiana na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia, lakini watu 80 wamekaidi kulipa kodi hiyo, hivyo wamefikishwa baraza la ardhi kwa awamu mbili.

"Watu hawa wamekaidi kulipa kodi ya ardhi ndio maana tumewafikisha baraza la ardhi, ili mali zao ziuzwe na watabeba gharama za kesi mahakamani pamoja na gharama za kuwalipa madalali watakaouza mali zao ili serikali ipate mapato,"alisema.

Naye Mwanasheria Msaidizi Ofisi ya Ardhi Kanda ya Kaskazini, Rosemary Mshana alisema kwa mujibu wa sheria ya ardhi namba 50 (4) ya mwaka 1999 kinachosema ili kutaifisha mali kwa wananchi wakaidi ni lazima upate kibali mahakamani na kibali hicho kimepatikana kupitia kwa Mwenyekiti Kiongozi wa Baraza la Ardhi, Fadhil Mdachi ili kusimamia maamuzi na kuwakabidhi madalali waliochaguliwa na mahakama kwaajili ya kuanza zoezi hilo.

Alisisitiza kuwa awamu ya kwanza wadaiwa 40 watalipa Sh. bilioni 1.1 huku awamu ya pili ya wadaiwa wengine 40  watalipa Sh. bilioni 1.2 na kusisitiza wananchi kulipa kodi ya ardhi ili kuepuka usumbufu.

Naye Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Kihamia alisema kuwa ni vyema wananchi wakalipa kodi ya ardhi ili kuepuka usumbufu wa kupelekwa mahakamani na kugharamia madalali wanaoshika mali na kuziuza ili kufidia deni wanalodaiwa na serikali.


No comments:

Post a Comment