Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha.
MAMLAKA ya Mapato nchini
(TRA), Mkoa wa Arusha imewataka wananchi wanaofanya manunuzi mbalimbali kudai
risiti ya malipo ili kuepuka kutozwa faini ya Sh. 30,000.
Aidha, TRA imeweka wazi
kwa upande wa wafanyabiashara watakaodakwa wameuza bidhaa zozote bila kutoa
stakabadhi kwa mnunuzi watalazimika kulipa faini ya Sh. Milioni 3.
Agizo hilo lilitolewa
mjini hapa juzi na Meneja wa TRA Arusha, Apili Mbarouk kwenye kikao
kilicholenga kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kulipa kodi kilichohudhuriwa na
Mkuu wa mkoa huo Mrisho Gambo.
Akizungumza kwenye kikao
hicho Mbarouk alisema, zoezi endelevu la ukaguzi kwa wafanyabiashara wanaouza
bidhaa mbalimbali limelenga kuhakikisha kila mwananchi anatimiza wajibu wake
kwa maslahi ya taifa.
“Tumeanza ukaguzi kwenye
maeneo yote ya Mji wa Arusha ili kuhakikisha wafanyabiashara wanatoa risiti
wanapouza bidhaa. Lakini pia wananchi wanaonunua nao pia wazidai,” alisema
Mbarouk na kuongeza:
“Kwa mfanyabiashara
atakayebainika hajatoa risiti atapigwa faini ya Sh. Milioni 3, huku mwananchi
ambaye amenunua bidhaa bila kudai risiti hiyo atatozwa faini ya Sh. 30,000,”
alisema.
Mbarouk akielezea kuhusu
kodi ya majengo alisema hadi Mei, Mwaka huu, walikuwa wamekusanya Sh. Bilioni
1, na kwa siku zilizobaki kabla ya mwaka wa fedha wa 2016/17 kukamilika
wanatarajia kukusanya zaidi.
“Tumejipanga zaidi
kukusanya kwenye maeneo yasipimwa na kufanyiwa uthamini ambako wamiliki
watalipa Sh. 15,000 kwa mwaka na maeneo yaliyopimwa wamiliki wanalipa kadiri ya
thamani ya jengo husika,” alisema.
Kwa upande wake Gambo
akielezea kuhusu kodi hiyo ya majengo alisema, endapo wadaiwa wote sugu katika
Jiji la Arusha wataendelea kukaidi kuilipa watafikishwa mahakamani kuanzia
Julai Mwaka huu.
Alisema wamiliki wa
majengo wanatakiwa kulipa kodi hiyo kwa mujibu wa sheria, kwani mapato hayo
yanahitajika kwa ajili ya kuendesha na kutekeleza miradi mbalimbali ya
maendeleo inayowahusu wananchi wenyewe.
“Hali si ya kuridhisha
wengi hawajajitokeza. Muda uliowekwa unaelekea ukikongoni mwisho Juni 30, Mwaka
huu.Baada ya hapo sheria zitachukuliwa kwa watakaobainika kuiibia Serikali
mapato ya majengo wanayoyamiliki.
“Haiwezekani umiliki
nyumba ugome kulipia kodi,natoa rai kulipia kwa hiari baada ya hapo faini
itakuwa mara tano ya kiasi ulichotakiwa kulipa au kupelekwa mahakamani kwa
mujibu wa sheria,” alisema Gambo.
Kufanyika kwa kikao hicho
kulilenga kuhakikisha mapato ya Serikali yanaendelea kukusanywa kwa ufanisi ili
kufikia malengo waliyojiwekea.
No comments:
Post a Comment