Na
MWANDISHI WETU
-ARUSHA
HALMASHAURI
ya Jiji la Arusha imefanikiwa kupeleka wanafunzi 578 Kidato cha tano kutoka
katika Shule zake za Sekondari 23.
Jiji
la Arusha lipo Kaskazini mwa Tanzania likiwa ndio kioo cha sekta ya
utalii na kituo cha biashara ya madini ya Tanzanite yanayochimbwa
Mirerani, Simanjiro mkoani Manyara.
Akielezea
kuhusu mafanikio ya kupeleka wanafunzi wengi Kidato cha Tano, Mkurugenzi
Mtendaji wa Jiji la Arusha Athuman Kihamia amewataka walimu kuongeza bidii ya
kufundisha na kutobweteka kwa matokeo ya sasa.
“Niwaombe
walimu waongeze bidii ili uwekezaji unaofanywa na serikali uakisiwe katika
ufaulu wa watoto, nisisitize pia kwa wazazi na walezi waendelee kutoa
ushirikiano kwa walimu ili kusukuma mbele gurudumu hili la elimu kwa watoto
wetu.
Nao
baadhi ya wazazi waliobahatika kuzungumzia matokeo hayo wameishukuru serikali kwa
kuendelea kuhakikisha elimu bora inatolewa kwa watoto wao.
“Tunamshukuru
Rais Dk. John Magufuli kwa sera yake ya elimu bure hakika imekuwa nguzo kwetu
sisi wazazi. Lakini pia kupitia wasaidizi wake Mkuu wa Mkoa Mrisho Gambo, Mkuu
wa wilaya Fabian Daqqaro na Mkurugenzi wa Jiji Kihamia,” alisema Mzazi Johari
Lyimo mwenye mtoto katika Shule ya Sekondari Kaloleni jijini hapa.
Kwa
miaka mingi sas Jiji la Arusha limekabiliwa na changamoto katika sekta ya
elimu, hatua ambayo serikali kupitia kwa Mkurugenzi wa Jiji imeendelea kutoa
majawabu kwa changamoto mbalimbali.
Baadhi
ya changamoto zinazotajwa kutatuliwa ili kufikia matokeo bora ni pamoja na kulipa
madeni ya walimu kupitia mapato ya ndani, kuongeza vyumba vya madarasa 147 kwa Shule
ya Msingi na Sekondari.
Nyingine
ni ukarabati wa vyumba 27 vya madarasa kwa kipindi cha miaka miwili na
kuhakikisha kila Shule ya Sekondari inakuwa na maabara yenye vifaa vyote.

No comments:
Post a Comment