Monday, June 12, 2017

MUINGILIANO MIGODINI MIRERANI YATISHIA UHAI WA WACHIMBAJI WADOGO

Na ELIYA MBONEA
-ARUSHA 

KAMPUNI ya Tanzanite One na Shirika la Madini nchini (STAMICO), wanaochimba madini ya Vito ya Tanzanite wametakiwa kutowarudisha nyuma zaidi, wachimbaji wadogo pindi wanapotoboza eneo la Delta linalomikiwa kisheria na mwekezaji huyo.

Wito huo ulitolewa mjini hapa juzi na Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini Adam Juma alipozungumza na MTANZANIA kuhusu usalama migodini, uzingatiaji mipaka, sheria na umuhimu wa ramani ya uchimbaji (mining plan).

Kauli hiyo ameitoa huku tayari baadhi ya wachimbaji wadogo wakiripotiwa kupigwa mabomu ya machozi chini ya ardhi, kunyang’anywa vifaa vya kazi na Wakaguzi wa mwekezaji wanaoshirikiana na askari polisi waliopo kituo cha mgodini. 

Akifafanua mitobozano ya wachimbaji wadogo waliopo Kitalu D dhidi ya Mwekezaji aliyepo Kitalu  C, Juma alisema tangu Mei mpaka Juni, Mwaka huu kumekuwa na muingiliano mkubwa kutokana Tanzanite One kuanza uzalishaji katika eneo la Delta.

“Wachimbaji wadogo wanachimba eneo la Delta kwasababu hakuna kikwazo chochote kwa vile muhusika wa eneo hilo kisheria alikuwa halichimbi. Lakini sasa ameanza kufanya uzalishaji kwenye eneo hilo,” alisema Juma na kuongeza:

“Tunasisitiza kwa Tanzanite One wasiwanyang’anye kabisa maeneo au kuwarudisha nyuma zaidi kunapotokea mtobozano, kwasababu bado taarifa ya Kamishna wa Madini kupitia Kamati ya kuangalia upya ramani zote mgodi hapo haijatoka,” alisema.

Akitoa mifano ya mitobozano ya hivi karibuni kwa wachimbaji wadogo wa Kitalu D, Kamishna Msaidizi Juma alisisitiza majadiliano yanayolenga kuimarisha usalama migodini hususani kwa wakaguzi wa mwekezaji.

“Shafti ya Delta inayoongelewa ipo mpakani na Kitalu D kama Mita 100 kutoka mpaka wa Kitalu C.Tunasisitizamajadiliano zaidi mfano mwekezaji akikuta umetoboza mpaka kwake anaweza kukurudisha nyuma zaidi Mita 20 kwa usalama ambayo bado ni kumpa upendeleo mchimbaji mdogo,” alisema Juma.

Alisema kutokana na sheria kutoa maelekezo kwa kila mchimbaji kufuata mipaka yake, aliwataka wachimbaji wadogo kuondoa dhana kuwa chini ya ardhi hakuna mipaka ya uchimbaji huku akiwasisitizia wabadili muelekeo na fikra za uchimbaji kuelekea Kitalu C ikiwamo kuwa na ramani ya uchimbaji (mining plan).

Alisema Mei Mwaka huu, kupitia kikosi kazi walipima migodi yote inayozunguka Kitalu C, yaani kitalu C na B ili wapate ramani ya pamoja itakayowezesha kuangalia hali ya muingiliano.

“Ripoti imekabidhiwa kwa Kamishna wa Madini na Mkaguzi Mkuu wa migodi, tunasubiria uamuzi. Tulichokiona ni muingiliano mkubwa kwani wengine wamechimba mita 200 lakini wametoka nje ya eneo lao mpaka Mita 1,000 kuelekea KIA,” alisema Juma.

Kwa upande wake mmliki wa mgodi namba 0000049 uliopo Kitalu D, Theresia Wapalila alisema,wafanyakaz wa mgodi wake walivamiwa na watu wenye silaha za moto kisha kuwapiga na kuwanyang’anya vifaa vya kazi.

“Watu hawa walivunja grill inayotenganisha mgodi wetu kupitia bomba ambalo hatujui nani aliliweka,” alisema Wapalila.    

Aidha taarifa ya ukaguzi uliofanywa na wajumbe wa kamati ya usuluhishi ilibaini kuwa mgogoro huo ulitokana na kukusudiwa na wafanyakazi wa Tanzanite One waliochungulia uelekeo wa mgodi a Wapalila.

Naye Mkurugenzi Mwenza wa Kampuni ya Tanzanite One Faisal Juma akizungumzia malalamiko hayo alikiri kuwapo kwa malumbano.

Makubwa maeneo ya machimbo hususani wachimbaji wadogo ambao kwa asilimia kubwa wameshindwa kutambua mipaka na kuheshimu sheria.

 “Mgodi wa Tanzanite One si wa kwetu peke yetu pale tunachimba kwa ubia na Serikali kupitia STAMICO.Hivyo ni lazima kuwepo na usimamiaji makini wa kulinda mipaka na kuhakikisha maslahi ya umma yanalindwa,” alisema Juma na kuongeza:

Eneo la Delta lipo kwenye lesesni ya Kitalu C kinachomilikiwa kisheria na kampuni. Ni kweli wachimbaji wadogo katika harakati za kuchimba wanapitiliza na kuingia eneo hilo. Sisi na serikali kwa pamoja tunayo haki ya msingi kusimamia maeneo hayo.

“Hakuna namna mchimbaji anaweza kuepuka usalama mgodini ndio maana kila mchimaji lazima awe na ‘mining plan’ yake,” alisema.


Mwisho.

No comments:

Post a Comment