Tuesday, May 30, 2017

HOSPITAL TEULE YA Dareda YAHITAJI MASHINE YA KUZUIA DAMU WAKATI WA UPASUAJI



Na ELIYA MBONEA
-BABATI

HOSPITAL ya Dareda inayohudumia wagonjwa zaidi ya 150 kwa siku kutoka maeneo ya Halmashauri ya wilaya ya Babati vijijini, mkoani Manyara haina mashine ya kuzuia damu wakati wa upasuaji.

Aidha, hospitali hiyo inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbulu, ikiendeshwa kwa ubia na Serikali inakabiliwa pia na upungufu wa vyandarua, mablanketi na mashine ya Ultra Sound.

Changamoto hizo zilibainishwa juzi hospitalini hapo wakati wa hafla ya kukabidhi msaada wa mashuka yaliyotolewa na Mfuko wa Mafao ya Kustaafu wa (GEPF) na Mwenyekiti wa Bodi Joyce Shaidi.

Akizungumzia changamoto hizo Mganga Mfawidhi Dk.Abraham Laizer alisema,hospitali hiyo yenye vitanda 200 vya kuandikishwa kwa sasa ikabiliwa na ongezeko kubwa la wagonjwa.

“Tuna mahitaji makubwa ya vifaa ambavyo kama tungevipata nahakika juhudi zetu za kusaidia na kuokoa maisha ya wananchi zingefanikiwa zaidi,” alisema Dk. Laizer na kuongeza:

“Mahitaji yetu sana ni mashine ya kuzuia damu wakati wa upasuaji na Ultra Sound. Kwa msaada huu wa msahuka hakika tunawashukuru hasa ukiwa umeelekezwa kwa mama na watoto,” alisema.

Alisema hospitali hiyo inapokea wagonjwa wa nje na wakulazwa ambapo wazazi wengi wamekuwa wakitumia kama kimbilio lao.

Alisema kutokana na mazingira ya baridi yaliyopo kwenye eneo hilo jamii hasa watoto wamekuwa wakikabiliwa na magonjwa ya Nimonia, magonjwa ya njia ya hewa pamoja na majeraha kwa watu wa pikipiki na wakulima.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya GEPF Shaidi alisema, mashuka 100 wameyatoa kwenye hospitali hiyo kama sehemu ya kurudisha faida kidogo kwa jamii.

“Tukiwa Mfuko wa Pensheni huwa tunatoa mafao kwa ajili ya uzazi na kusaidia huduma kwa mama baada ya kujifungua, tuliona hapa mna upungufu wa mashuka kwa mama wajawazito baada ya kujifungua na watoto,” alisema Shaidi.

Naye Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Padri Peter Salahoo, alisema hospitali hiyo ilianzishwa Mwaka 1947 na Shirika la Masista kisha kukabidhiwa kwa Askofu wa Jimbo la Mbulu.

“Tupo hapa kushirikiana na Serikali kuisaidia jamii tunatoa huduma mbalimbali ikiwamo matibabu bila malipo kwa mama na mtoto chini ya miaka mitano pamoja na wazee zaidi ya miaka 60.

“Eneo hili ni la baridi kwa ujumla mahitaji bado ni mengi hasa kwa upande wa mashine kama Ultra Sound ambazo huwasaidia madaktari kutambua mahitaji ya kina mama pamoja na kuangalia mtoto anaendeleaje tumboni,” alisema Padri Salhoo na kuongeza:

“Tunashukuru msaada huu wa GEPF lakini tunawaomba na wadau wengine watupie macho maeneo haya ya hospitali za vijijini,” alisema.

Katika hatua nyingine hospitali hapo mara baada ya kutembelea na kujionea mahitaji mengine naye Dk.Joseph Roli aliushukuru mfuko huo kwa msaada wa mashuka kutokana na kukabiliwa na upungufu wa shuka za kutandika vitandani.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment