Thursday, December 1, 2016

FILAMU YA KIJERUMANI KUUTANGAZA UTALII NCHINI

Na FILBERT RWEYEMAMU

SERENGETI

Sekta ya Utalii nchini inatarajiwa kupiga hatua mbele katika kipindi cha mwaka mmoja ujao baada ya kampuni ya Polyphon Film kutoka nchini Ujerumani kurekodi filamu zinazotangaza vivutio vya utalii nchini.

Mkurugenzi wa Utalii na Masoko wa shirika la Hifadhi za Taifa nchini(TANAPA), Ibrahim Mussa alisema juzi wakati kampuni hiyo ikikamilisha sehemu ya utengenezaji wa filamu yake nchini kuwa kampuni hiyo hutengeneza filamu zinazoelimisha jamii ambazo ni endelevu kama ulivyo mchezo wa Isidingo unaorekodiwa nchini Afrika Kusini.

"Kipindi cha mwaka mmoja tutaona matokeo ya hii filamu ambayo ina watazamaji wengi katika nchi za Ujerumani,Uswizi na Austria tunaamini maeneo yaliporekodiwa yataijenga sana nchi yetu na kukuza utalii wetu kwa ujumla,"alisema Mussa

Alisema kuvichagua vivutio vya hapa nchini ni ishara kuwa sekta ya utalii Tanzania imekua ikijipatia sifa njema hasa kaipindi hiki ambacho serikali ya wamu ya tano imepania kuipa nafasi ya kuongeza mapato nchini.

Naye Mratibu wa Uzalishaji wa kampuni ya Polyphon,Mona Lessnick alisema wamevutiwa kufanyia kazi zao nchini katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti,hifadhi ya Taifa ya Arusha na eneo la hifadhi ya Jamii ya Enduimet wilayani Longido.

Miongoni mwa waigizaji maarufu ni Hardy Kruger na John Wayne ambao wamejiptia umaarufu mkubwa duniani.

"Tutaanza kuonyesha programu zetu kuanzia kipindi cha Pasaka mwakani kwenye kituo cha Runinga cha ZDF nchini Ujerumani tunaamini karibu watazamaji 10 milioni wataona namna Tanzania ilivyobarikiwa na rasilimali nyingi na kutembelea vivutio hivyo,"alisema Mona

Alisema gharama ya kutengeneza filamu hiyo imegharimu zaidi ya Sh 400 milioni ambazo sehemu kubwa imetumika nchini na walikua na idadi ya watu 50.

mwisho



No comments:

Post a Comment