Na ELIYA MBONEA
-MANYARA
MAKAMANDA wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) kutoka
Kata 18 za wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wameapa kumng’oa Mbunge wa
Chadema James Ole Millya ifikapo Mwaka 2020.
Kauli hiyo wameitoa juzi wilayani hapa mbele ya Kaimu Katibu Mkuu
wa UVCCM Taifa Shaka Hamdu Shaka aliyekuwa wilayani humo kwa ajili ya shughuli
za kikazi.
Akitangaza msimamo huo kwa niaba ya Makamanda hao, Kamanda wa
UVCCM wilaya ya Simanjiro Daniel Ole Materi alikiri kwamba uchaguzi wa Mwaka
2015 waliteleza hivyo wameshafahamu kosa na sasa hawatarudia.
Alisema jukumu na mikakati wanayoendelea kuifanya kwa sasa ni
kuhakikisha Chama chao kinarejesha heshima yake kwa wananchi wa Jimbo hilo
baada ya kuwa imechukuliwa na mtu asiyedhamini wala kujali wananchi wa
Simanjiro.
“Mpaka sasa tuna imani kubwa kwa wananchi inayojengwa na utendaji kazi wa Rais Dk. John Magufuli. Tuna kila sababu kwa CCM na Jumuiya zake kulirudisha jimbo hili,” alisema Materi.
Kiongozi huyo wa UVCCM wilaya aliendelea kueleza kwamba kwa
wananchi wa wilaya hiyo wanayo majuto makubwa baada ya kuwa wamemchagua Mbunge
Ole Millya.
“Wananchi walitegemea kuona lolote baada ya kuwa Millya
amechaguliwa sasa simekuwa tofauti na matarajio yao kwani wamegundua hana uwezo
wa mbinu za kuwatumikia,” alisema Materi na kuongeza:
“Tumejipanga kuhakikisha Kata Saba zilizochukuliwa na Chadema zinarejea CCM,” alisema
Kwa upande wake Shaka akizungumza na Makamanda hao aliwataka
kuhakikisha wanathamini kiapo walichokula ambapo aliwahidi kuwa ahadi
waliyopitoa kwake atawaisilisha kwa Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana .
Pamoja na mambo mengine waliyoyawasilisha kwake, Shaka aliwataka kujiandaa kushiriki katika chaguzi za jumuiya zinazotarajiwa kufanyika mwakani huku akiwahimiza vijana wilayani humo kujitokeza kuwania nafasi hizo za uongozi wa jumuiya.
“Katika uchaguzi huu tumejipanga kuhakikisha mchujo unakuwa mkali ili kujua nani ana sifa za kuwa kiongozi wetu badala ya kupitisha mpaka watu walioshiriki kutuuza mwaka 2015, alisema Shaka aliyehitimisha ziara yake kwa kuzindua jengo la ofisi za UVCCM lenye thamani ya Sh Milioni 10.3.
Naye Mwenyekiti wa UVCCM wilayani humo Kiria Laizer alisema tayari
mkakati wa kupata ushindi katika jimbo hilo umekamilika kilichobakia kwa sasa
ni kusubiria Mwaka 2020 ili Mbunge Millya afungashiwe virago vyake na wananchi
kupitia sanduku la kura.
Katika ziara hiyo ya siku tatu ilimuwezesha kiongozi huyo wa
kitaifa wa UVCCM kufungua mashina mapya ya Chama hicho ikiwamo kugawa kadi kwa
wanachama wapya wa Kata ya Naberere na kuzungumza na wana CCM.
MWISHO
No comments:
Post a Comment