Na ELIYA MBONEA
-MONDULI
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU), mkoani Arusha imeagizwa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani
watu wanaodaiwa kutafuna Sh Milioni 448.9 za mradi wa Machinjio ya Manyara
Ranch yaliyopo wilayani Monduli mkoani hapa.
Agizo hilo lilitolewa wilayani hapa
juzi na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo wakati wa ziara yake ya kutembelea
mradi huo wa machinjia ya kisasa uliomo ndani ya shamba lenye ukubwa wa hekari
44,930.
Akiwa ameongozana na Mbunge wa Jimbo
hilo (Chadema), Julius Kalanga, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo (Chadema), Isack
Joseph na viongozi wengine Gambo alishangazwa kuona mradi huo ulioanza Mwaka
2009 ukiwa haujakamilika ilhali fedha zilishatolewa.
Alisema zaidi ya Sh Milioni 448.9
zilishatolewa kwa ajili ya gharama za ujenzi ikiwamo jengo la machinjio zaidi
ya Sh Milioni 223.5, ununuzi wa vifaa vya kisasa.
“Fedha zilizotolewa na wafadhili
Shirika la Misaada la Marekani (USAID), kupitia Shirika la African Wildlife
Foundation (AWF), zimeliwa na wachache wakiwamo wa Wizara ya Mifugo na Kilimo.
Hili hatutalivumilia,” alisema Gambo na kluongeza:
“TAKUKURU mnapaswa kuchukua hatua kwa
kuwasaka wote waliohusika kukwamisha huu mradi wafikisheni katika vyombo vya
sheria wakajibu tuhuma zao,” alisema.
‘’Haiwezekani watu wanakula fedha
za wafadhili ambao wana nina nzuri na nchi halafu tunawaacha hilo sio kwa
serikali hii ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt John
Magufuli’’
‘’Lazima waliokula fedha za wafadhili
wanapaswa kukamatwa mara moja na hiyo nawaachia TAKUKURU ndani ya siku chache
zijazo nahitaji majibu kuwa wamekamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu
mashitaka yao’’ alisema Gambo.
Kwa upande wake Meneja wa AWF Fidelis
Ole Kashe alilitaja lengo la kujengwa machinjio hiyo kuwa ilikuwa ni kupanuaa
wigo wa vyazo vya mapato yanayotokana na kuuza mifugo na nyama bora katika
kiwanda.
Alisema kiwanda hicho cha machinjio
kililenga kutoa soko la kuuza mifugo na nyama kwa vijiji vinavyozunguka
machinjio hiyo ikiwamo ajira itakayotolewa kwa wananchi hususani kwa jamii
zilizo jirani.
“Upungufu uliopo katika mradi huo ni
kutolewa fedha nyingi lakini hadi sasa mradi umeshindwa kukamilika, kukosekana
kwa mwekezaji, vifaa vilivyotumika kujenga havina ubora,” alisema Kashe na
kuongeza:
“Mradi huu haukuwa umewekewa mipango
endelevu ambapo wafadhili walisitisha kutoa fedha tena kwa ajili ya kumalizia
mradi husika wakati fedha zilizokuwa zimetolewa zikiwa hazina maelezo ya jinsi
zilivyotumika.
Mwisho
No comments:
Post a Comment