Wednesday, November 23, 2016

UJERUMANI YAMWAGA ZAIDI YA BILIONI 60 EAC

Na ELIYA MBONEA
-ARUSHA

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC), imepokea msaada wa Euro Milioni 40, zaidi ya Sh Bilioni 60 kutoka nchi ya Ujerumani kwa ajili ya mradi wa afya hususani chanjo kwa watoto na Maabara. 

Akizungumza mjini hapa jana yalipo Makao Makuu ya EAC, wakati wa kusaini mkabata huo, Balozi wa Ujerumani nchini, Egon Kochanke alisema, ni fahari ya nchi yake kuendelea kuisaidia Jumuiya hasa katika suala la afya. 

Alisema kiasi hicho chga fedha kimetolewa na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW), kushrikiana na Serikali ya nchi hiyo. 

Alisema msaada wa Euro Milioni 30 ulitolewa umelenga kusaidia suala la utoaji wa chanjo kwa watoto katika nchi hizo za Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Jumuiya hiyo inaundwa na nchi wanachama ambazo ni Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi na Sudani Kusini ambaye ni mwanachama mpya aliyepokelewa hivi karibuni. 

“Kampeni hii ni kubwa katika eneo hili, tutaendelea kutoa misaada, kama ambavyo tumekuwa tukishiriki kusaidia mambo mengi huko nyuma,” alisema Balozi Kochanke. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa KfW, Dar  es Salaam Dk. Helmut Schon alisema Euro Milioni 10 zilizotolewa zimelenga kusaidia Maabara kwa nchi hizo wanachama wa EAC.

Dk. Schon alisema, KfW imetoa msaada huo kwa lengo la kusaidia ikitambua kwamba pamoja na mipaka ya nchi na nchi iliyopo bado magonjwa yamekuwa hayana mipaka katika kuyashughulikia. 

“Mkataba tunaosaini leo wa Euro Milioni 30 unaendeleza mchango kutoka Ujerumani kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaofikia Euro Milioni 90 tangu Mwaka 2013,” alisema Dk. Schon. 

Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Liberath Mfumukeko alisema msaada huo ni muhimu kwa jumuiya hiyo hasa katika suala zima la afya. 

“Msaada huu ni muhimu kwa nchi wanachama wa EAC kwa suala la afya bado ni changamoto kubwa. Kwa niaba ya wananchi wa jumuiya yetu naishukuru sana Serikali ya Ujerumani,” alisema Balozi Mfumukeko. 

Katika makabiadhiano hayo Balozi Mfumukeko  alimuahidi Balozi wa Ujerumani Kochanke pamoja na Mkurugenzi wa KfW Dk. Schon kuwa watahakikisha msaada huo unakwenda kutekelezwa kama ilivyokusudiwa na wahisani. 

“Tutahakikisha tunafanya kila jitihada kuona mradi huu unafanbikiwa kwa nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Balozi Mfumukeko. 


Mwisho. 

No comments:

Post a Comment