Wednesday, November 23, 2016

SAMIA SULUHU: AFRIKA IMEPIGA HATUA HAKI ZA BINADAMU, WANAWAKE

Na ELIYA MBONEA
-ARUSHA

BARA la Afrika limetajwa kuwa na mwamko mkubwa katika kutekeleza Haki za Binadamu na hasa haki za Wanawake.

Aidha, changamoto iliyopo imetajwa kuwa upande wa sekta binafsi hasa katika Bodi za Mashirika zenye uamuzi ambazo kwa namna moja ama nyingine zimeendelea kuwa na wanawake wachache.

Akizungumza mjini hapa jana wakati wa ufunguzi wa kikao cha ngazi ya juu cha Umoja wa Afrika kuhusu Haki za Binadamu, Makamu wa Rais Samia Hassan Suluhu alisema, Afrika ikiwamo Tanzania zimeendelea kuteleza matamko yanayosisitiza utekelezwaji wa haki kwa wananchi wake.

Alisema mwamko wa Bara la Afrika katika kutekeleza Haki za Binadamu na hasa za wanawake umeendelea kuwa mkubwa tofauti na miaka ya nyuma.

“Bado kuna changamoto hasa katika sekta binafsi wanawake katika Bodi za maamuzi za Mashirika idadi yao ni ndogo,” alisema Mama Samia na kuongeza:

“Tunaendelea kulifanyia kazi hili na sekta binafsi wenyewe wamekuwa wakilifanyia kazi ili kuongeza idadi ya wanawake kwenye Bodi hizo,” alisema.

Alisema katika utafiti uliofanyika umebaini kuwa Bodi zenye wanawake zimekuwa na utendaji kazi mzuri zaidi ikilinganishwa na maeneo mengine ambayo wanawake hawapo.

Akizungumzia kuhusu umuhimu wa utolewaji wa haki kwa mwanadamu alisema zipo haki mbalimbali ambazo zimeanishwa kama haki za msingi na lazima kutolewa kwa wananchi.

Alisema kumekuwapo na matamko kwa nchi za Afrika katika kutoa elimu kwa watu wake, ambapo kwa hapa nchini Serikali imekuwa ikitekeleza unaoji wa haki ya kupata elimu kwa kila Mtanzania.

Alisema katika utekelezaji huo nchi ya Tanzania imeweza kupiga hatua zaidi kwa kuhakikisha elimu ya kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha Nne inatolewa bure.

“Hatua hii imelenga kuhakikisha kila Mtanzania anaingia darasani na kusoma. Bado pia tumeendelea kuboresha elimu kwa kutekeleza mambo mbalimbali,” alisema Mama Samia.

Katika utekelezaji huo Makamu wa Rais alisema kwamba suala la haki ya afya kwa binadamu nalo limeendelea kutekelezwa na Serikali za Afrika ikiwamo Tanzania.

“Serikali zetu zimeendelea kutoa matamko kadhaa ikiwamo kutekeleza na Azimio la Abuja linalotaka asilimia ya bajeti ya afya kwa kila nchi ifikie asilimia 15.

“Tanzania tupo kwenye asilimia 10 na tunaelekea kwenye asilimia 15. Juhudi zetu za kuendelea kujenga Zahanati kila Kijiji, Hospitali za Kata na wilaya zimelenga kuhakikisha Mtanzania hasa mwanamke anapata afya ya mwili,”alisema Mama Samia.

Akifafanua zaidi kuhusu haki za Wanawake hasa katika ngazi za uamuzi alisema awali wanawake hawakuwa wakiingia kwenye maeneo hayo, ambapo baada ya matamko Beijingi kuanza kutekelezwa wanawake walianza kuonekana.

Alisema kwa upande wa nchi ya Tanzania yenyewe imeweza kupiga hatua zaidi kwa kufikia mpaka asilimia 30 kimatamko huku ukweli halisi ukitajwa kuzidi asilimia hiyo.

“Kwa kweli mpaka sasa tumeshaizidi hiyo asilimia 30. Lakini Katiba Mpya itakapopitishwa tunaamini itakuwa ni asilimia 50 kwa 50 katika ngazi za uamuzi. Hii itakuwa ni kutekeleza wajibu wa kumpa haki mwanamke,” alisema Mama Samia.

Kwa upande wake Rais wa Mahakama hiyo, Jaji Sylvain Ore, alisema kongamano hilo la miaka 10 lililohudhuriwa na wajumbe 150 linatarajiwa kuja na mapendekezo yatakayokuza utendaji wa shughuli za Mahakama hiyo kwa siku zijazo.
Mwisho.


No comments:

Post a Comment