Na ELIYA MBONEA
-ARUSHA
SPIKA wa Bunge la Tanzania Job Ndugai, ametakiwa kuanza kuchukua
hatua za kufanya marekebisho ya baadhi ya Kanuni za Bunge ili liweze kutenda
haki.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mbunge wa Jimbo la
Moshi Vijijini (Chadema), Anthony Komu baada ya Mahakama ya Haki ya Afrika
Mashariki (EACJ), kutoa hukumu ya Rufaa iliyofunguliwa na Serikali dhidi ya
ushindi wa Komu.
Alisema kutokana na uamuzi uliotolewa na Mahakama hiyo,
Serikali ya Tanzania haipaswi kuendelea kusubiria mpaka ikamatwe, badala yake
inapaswa kufanya marekebisho ya kanuni ili haki iwe inatendeka.
“Kwa sasa mimi ni Mbunge sina
haja ya kufanya ligi dhidi ya Serikali au Bunge. Baada ya matokeo haya
nimepanga kumwandikia barua Spika wa Bunge kuwambia sasa anapaswa anapaswa kuchukua
hatua zinazotakiwa.
“Spika ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya
Kanuni kwa hiyo baadhi ya Kanuni zinapaswa kurekebishwa ili zioane na ambacho
kimesemwa hapa mahakamani.
“Kimsingi ukienda kwenye hitimisho
unaweza kusema matokeo si nzuri kwasababu Mahakama imesema mtu binafsi baada ya
ile kesi ya Professa Anyang’ Nyong’ wa Kenya hawezi kuleta tena shauri
linalofanana na hilo mbele ya Mahakama hii.
“Lakini ukienda kwenye mchakato wenyewe
na hoja ambazo wameziwasilisha utaona kuna faida kubwa ya shauri hili
kusikilizwa mpaka hapa lilipofikia. Hatujapoteza kitu ni mahali pazuri, uongozi
wa bunge na nchi unapaswa kuchukua hatua za makusudi ili kuondokana na hali
kama hiyo,” alisema Komu.
Komu wakati akifungua shauri hilo alikuwa
bado hajachaguliwa kuwa Mbunge wa Moshi Vijijini alisema, kuchukuliwa kwa hatua
hizo za serikali kutasaidia mtu mwingine asifungue shauri kama hilo kwenye
Mahakama ya EACJ.
Na akilipeleka shauri hilo kwenye
Mahakama ya TZ lazima Mahakama ya Tanzania ililete hapa EACJ kwa ajili ya
kuomba tafsiri itakayorudishwa kwenye mahakama ya Tanzania kuendelea na shauri.
“Shida hapa ilikuwa ni mtu binafsi
ameleta shauri hili na si Taasisi kwa maana nyingine ingekuwa Mahakama ya
Tanzania imeomba, Bunge au Serikali maana yake shauri hili lingesikilizwa na
hukumu ingetolewa.
“Sio siri kwamba majibu ya hukumu yanagekuwa
kama awali kwamba Bunge la Tanzania halikufanya uchaguzi kulingana na Mkataba
wa EAC unavyotaka katika Ibara ya 50,” alisema Komu aliyekuwa ameongozana na
Kaka yake Yasinti Komu pamoja na Kada wa Chadema Daniel Porokwa.
Kwa upande wake Wakili Edson Mbogoro
aliyekuwa akimwakilisha Komu katika shauri hilo alisema, Mahakama iliyotoa
Hukumu ya Rufaa hiyo haikuelekea kwenye stahiki za Rufaa badala yake
ilishughulikia suala la je Mahakama ya
awali ilikuwa sahihi kuipokea na kushughulikia malalamiko ya Komu?
Alisema kutokana na kupitia hoja
hizo Mahakama hiyo ilifikia hitimisho la
la kumuona Komu kama mtu binafsi ambaye anaelekezwa na Ibara ya 30 na 33 na 51 kuwa
alipaswa kuendelea na kesi hiyo aliyokuwa amefungua Mahakama Kuu ya Tanzania
Kanda ya Dodoma.
“Isipokuwa kama wangefikia upande wa kuomba
tafsiri ya Mkataba wa EAC basi Mahakama Kuu yenyewe ndio ingefanya marejeo
kwenye Mahakama ya EACJ lakini pia suala hilo bado lingeamuliwa na Mahakama Kuu
ya Tanzania,” alisema Wakili Mbogoro na kuongeza:
“Mahakama hii imesema karika rufaa haikuwa
sahihi kwa Mahakama ya awali kupokea na kusikiliza shauri hili. Lakini pia
imeweka wazi kwamba kwa vile shauri hili ni la muhimu si kwa Tanzania tu bali lina
manufaa kwa nchi zote za EAC, ndio maana katika uamuzi wao wameagiza kila upande
ubebe gharama zake za kesi,” alisema.
Hata hivyo Wakili Mbogoro alisema kuwa
uamuzi huo umefikiwa baada ya kesi ya Professa Anyang’ Nyong’ wa nchini Kenya
kuilazimu Jumuiya hiyo kufanyia marekebisho Mkataba wa EAC.
“Kabla ya kesi ya Prof Anyong’ kusingekuwa na tatizo kwa namna Komu
alivyowasilisha katika Mahakama hii,” alisema Wakili Mbogoro.
Komu alifungua kesi katika Mahakama ya Afrika Mashariki
akiomba itoe tafsiri ya kisheria juu ya Bunge la Tanzania akidai lilikiuka Ibara
ya 50 ya Mkataba wa EAC katika uchaguzi wa Wabunge wa Bunge la Afrika
Mashariki(EALA), Aprili 17, Mwaka 2012.
Katika kesi hiyo namba 7 ya Mwaka 2012, Jopo la Majaji
watatu Jean Bosco Butasi, Isaac Lenaola na Faustine Ntezilyayo lilimpa ushindi
Komu. Hata hivyo, Serikali haikukubaliana na uamuzi huo na kukataa Rufaa.
Rufaa iliyotolewa hukumu jana ilisikilizwa na Jopo la Majaji
watano wakiongozwa na Rais wa Mahakama hiyo Jaji Dk. Emmanuel Ugirashebuja,
Makamu wake Libore Nkurunzinza, Edward Rutakangwa, Aaron Ringera na
Geoffrey Kyiryabwirwe.
Awali Wakili Mkuu Mwandamizi wa Serikali, Mark Mulwambo,akisaidiana
na Pauline Mdendemi,walipinga na kudai mahakama hiyo ya EACJ haina uwezo wa
kisheria wa kutoa uamuzi kuhusu Bunge ambalo ni mwanachama wa EAC.
Mawakili wa Utetezi Edson Mbogoro na Wakili John
Mallya, walidai Mahakama hiyo ina uwezo wa kutoa tafsiri ya kanuni za uchaguzi
wa wabunge wa EALA.
"Mahakama hii ina uwezo wa kisheria wa kuto tafsiri
ya kanuni za uchaguzi wa wabunge wa EALA kama unafuata mkataba wa
uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.”alisema Wakili Mbogoro.
Wakili huyo aliiomba mahakama hiyo izuie mabunge ya
nchi wanachama yasijaribu kupindisha sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi wa
wabunge wa EALA kama ilivyofanywa na Bunge la Tanzania.
Mwisho
No comments:
Post a Comment