NA ELIYA MBONEA, ARUSHA
WAKILI maarufu
jijini Arusha Medium Mwalle na wenzake watatu wamesomewa mashitaka 42 yanahusiana
na utakatishaji wa Fedha, kugushi nyaraka na kukutwa na mali zilizopatikana kwa
njia za uhalifu.
Watuhumiwa hao walisomewa mashitaka ya awali jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha
mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mustapha Siyani kabla ya kesi hiyo haijapelekwa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha tayari kwa kusikilizwa.
Akisoma maelezo hayo ya awali Wakili wa Serikali Mkuu Oswald
Tibabyakyomya alidai mahakamani hapo kwamba, watuhumiwa hao walitenda makosa
hayo kati ya Mwaka 2009 hadi Mwaka 2011 kwa nyakati tofauti.
Alidai kati ya makosa hayo 42, mtuhumiwa wa kwanza Mwale
anakabiliwa na makosa 27 ikiwa ni pamoja na
kuficha uhalisia wa mali ambapo
anadaiwa kutumia Sh. Milioni 70 kununua shamba katika kijiji cha Ekenywa
Arumeru mkoani Arusha.
Wakili huyo alidai katika kuficha uhalisia wa mali
mtuhumiwa huyo anadaiwa kutumia Sh. Milioni 250 kununua gari aina ya BMW T. 907
BTS, Dola za Marekani 330,000 alizonunulia gari aina ya Landrover Discovery T.
643 BTS.
Aliendelea kudai kwamba mtuhumiwa huyo pia alinunua nyumba
mbili moja yenye thamani ya Dola za
Marekani 80,000, Kiwanja namba 22 kilichopo Ilkiurei Arumeru na Dola za
Marekani 300,000 alizonunulia nyumba namba 21 eneo la Njiro jijini Arusha
Wakili huyo wa Serikali aliendelea kudai kwamba Agosti 5,
2011 mtuhumiwa Mwale alikutwa na Hundi Tatu za Kimarekani zenye thamani ya Dola
10,302, Dola 10,333 na Dola 95,079 ambapo kutokana na mazingira Hundi
zilionekana kuibiwa ama zilipatikana kwa njia ya uhalifu.
Kwa upande wa Hakimu Mfawidhi Siyani aliwataka watuhumiwa
hao kutojibu lolote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza
kesi hiyo.
Katika kesi hiyo upande wa Serikali uliiambia Mahakama hiyo
kwamba umejipanga kuwasilisha mashahidi 41 na vielelezo zaidi ya 42 kutokana na
vingine kuendelea kuwasilisha. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Februari 2, Mwaka
huu ambapo upande wa Jamhuri watamalizia kuwasilisha vielelezo vya ushahidi
wao.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment