Wednesday, February 11, 2015

MWINYI: LOWASSA MUNGU ATAKUSAIDIA

NA ELIYA MBONEA, MONDULI .

RAIS mstaafu wa awamu ya pili Alhaji Ali Hassani Mwinyi amemuomba Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na Mbunge wa Monduli kuendelea kusaidia wananchi kwani na yeye Mungu atamsaidia.

Kauli hiyo aliitoa wilayani hapa juzi kwenye Jubilee ya miaka 20 ya Sekondari ya Wasichana ya Maasae aliyoifungua Mei 27, Mwaka 1995 ikiwa ni maalumu kwa wasichana wa jamii za wafugaji na waokota matunda.

Akizungumza katika Jubilee hiyo Rais mstaafu Mwinyi alisema, ni kawaida ya binadamu kufanya mema kwa ajili ya ujira.Lakini kwa alichokiona shuleni hapo kwa miaka 20 iliyopita ni wema usio na malipo kwa watoto wa Tanzania.

Kutokana na mabadiliko aliyoyakuta kutoka majengo mawili mwaka 1995 hadi Maabara Nne, Maktaba moja, madarasa 12, mabweni 11 na Zahati moja, Mzee Mwinyi aliwataka watu kuiga mfano wa Lowassa na Dk. Reginald Mengi.

“Lowassa endelea kusaidia katika kazi ya shule na wewe Mungu atakusaidia,” alisema Mzee Mwinyi na kuongeza:

“Niwaombe wadau wengine tusiwachie Lowassa na Dk. Mengi mzigo huu wa kusaidia elimu ndani ya jimbo hili na nchini kwani nao wakazi nyingi,” alisema.

Katika Jubilee hiyo Mzee Mwinyi alisikitishwa na hatua za kukataa kuwasomesha watoto wa kike zinazotekelezwa na baadhi ya wazee katika jamii za kifugaji na waokota matunda.

“Hili ni jambo la kusikitisha tumesaidiwa miaka 20, lakini bado ipo jamii inakataa kuwapa nafasi watoto wa kike kusoma badala yake wanawaozesha. Ni kwanini wazazi hawa hawaoni wivu watoto wengine wanapopata elimu?” Alihoji Mzee Mwinyi.

Awali Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Jimbo hilo alisema, wananchi wa Monduli wataendelea kumkumbuka Mzee Mwinyi kwa mambo mengi aliyowafanyia.

“Napata taabu kuzungumza kabla ya Mzee Mwinyi. Lakini nitajitahidi ili aone kuwa alinifundisha kazi vizuri, kwani katika utawala wake aliniteuwa kuwa Waziri wa Ardhi”.

“Katika utawala wake alitusaidia kuanzisha shule hii na alitoa hekari 700 kwa ajili ya Chuo Kikuu, lakini pia alichangia wakati huo Sh. Milioni 46 za kuanzisha Saccos ya Walimu Monduli,” alisema Lowassa.

Aidha Lowassa aliwapongeza pia wafadhili wa Oba kutoka nchini Marekani kwa kuiwezesha shule hiyo kuzalisha wasomi 1,001 ambayo ni nguvu kazi ya taifa.

“Hatuna maneno ya kuwashukuru kwa kazi kubwa na ya kipekee mliyoifanya katika taifa letu,” alisema Lowassa.

Kwa upande wake Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP Dk. Reginald Mengi aliyewahi kuchangia kiasi cha Sh. Milioni 200 katika sekondari hiyo alisema, Jubilee ya miaka 20 ni ya mafanikio makubwa.

“Hii si miaka 20 ya kawaida, ni Jubilee ya mafanikio makubwa sana kwetu, Mungu akikupa Baraka una kila sababu ya kuwasaidia na wengine.

“Nakushukuru sana Mbunge wa Monduli Lowassa umefanya makubwa Monduli na Tanzania . Mdogo wangu hongera sana kwa kazi kubwa unayoifanya,” alisema Mengi.

Naye Askofu Solomon  Masangwa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri  Dayosisi ya Kaskazini Kati katika Jubilee hiyo alisema kati ya wanafunzi waliomaliza shuleni hapo kutoka jamii za wafugaji na waokota matunda wapo walimu 200.

Alisema kila mwaka shule hiyo imekuwa ikichukua watoto 60 kutoka maeneo ya wafugaji ya Babati, Longido, Ngorongoro, Monduli, Simanjiro na Kiteto.

“Tunawashukuru sana wafadhili wetu wa ndani na nje ya nchi na hasa Mbunge Lowassa kwa kazi kubwa na michango unayoendelea kuitoa. Mungu aendelee kukuimarisha katika utumishi wako kwa kazi na nchi,” alisema Askofu Masangwa.


Mwisho. 

No comments:

Post a Comment