Wednesday, February 11, 2015

VIONGOZI AU WAMEJIPANGA KUNYONYA DAMU ZA WATU

JICHO LA ARUSHA


VIONGOZI wa nchi za Umoja wa Afrika (AU),wiki iliyopita wamekutana jijini Addis Ababa, nchini Ethiopia yalipo Makao Makuu ya Umoja huo.

Kwa miaka mingi wamekutana na kufanya mikutano wanayodai ni ya kuwainua wananchi Afrika kiuchumi, kimaendeleo na mipango imara ya usalama kwa maisha na mali za watu.

Pamoja na mikutano hiyo ya mara kwa mara kwa viongozi hawa, bado wananchi wengi wa Bara la Afrika hawajaweza kunufaika na mikutano ya wakubwa hawa.

Nikiangalia kwa Jicho la Arusha Bara la Afrika limeendelea kuwa mgodi wa mataifa tajiri kwa kutumia watu wao kuja Afrika na wakati mwingine kuwatumia viongozi wa AU kuchukua utajiri wa Afrika.

Kwa miaka mingi vizazi vya Afrika vimeendelea kuishi au kufa kutokana na umasikini, njaa na vita inayosababishwa na tamaa viongozi hawa kutaka kuendelea kuishi madarakani kwa kuiuza Afrika kwa wakubwa zao.

Kuwapo mambo mbalimbali yaliyojadiliwa katika mkutano, binafsi kunanielekeza kufananisha mkutano wa viongozi hao kama darasa la watoto (Baby Class) wanaopelekwa shuleni ili kucheza na kukuza akili zao.
Ukiitafakari Afrika jinsi lilivyobarikiwa utajiri wa rasilimali za misitu, mafuta, gas, dhahabu, almasi, makaa ya mawe, maji, vivutio vya utalii vya kila aina na watu wake, huwezi kupata jibu la umasiki kwa wananchi wake.

Lakini, ukiangalia kwa makini pia aina ya viongozi wanaokutana AU kwa ajili ya kuangalia maisha ya Afrika ijayo ni wazi kwamba utapata jibu kwanini Afrika, bado watu wake wameendelea kuwa maskini.

Jibu linalopatikana hapa baada ya kuangalia wingi wa rasilimali zilizopo Afrika, linajielekeza kwa viongozi wakuu wan chi za Afrika kwamba wao ndio chimbuko la umaskini wa bara hili na watu wake.

Hakuna mwingine anayesababisha Bara hili kuwa maskini wa kutupwa na kufanya wananchi kufa na njaa, eti kwasababu tu watu wawili wenye uroho wa madaraka wameshindwa kuelewana kuhusu mkate wao na familia zao.

Leo mapigano yaliyopo nchi za Afrika ukiachia vikundi vya kigaidi ambavyo vimekuja na mfumo wao wa kutafuta madaraka kwa kutanguliza Imani ya kidini, mapigano mengi yamesababishwa na tamaa za madaraka.

Ukiachia hayo, njoo hili la mkutano wa viongozi wakuu wa nchi za Afrika, binafsi naendelea kufananisha na “Baby Class” wanaotoka nyumbani kwenda kucheza shuleni kisha kusubiri kurudishwa majumbani mwao.

Pamoja na madaraka makubwa waliyonayo nadhani baadhi ya viongozi wengi bado hawajajitambua kama wanayo nafasi ya kutengeza jambo kwa manufaa ya watu wanaowangoza, badala ya kuwaza kuongozwa.

Nasema viongozi hawa bado wanaongozwa na mataifa tajiri, hainiingi akilini kuona bara lenye utajiri viongozi wake wakisubiria fadhila za nchi tajiri kuwachangia fedha ili wakutane kujadili maendeleo ya wananchi wao.

Hii ni aibu tena fedheha kwa mtu anayeunda kundi la viongozi wa AU kuendelea kuchangiwa fedha ili asafiri na ndege ya nchi yake, wafuasi wake kwenda makao makuu ya AU kujadili maendeleo, ni maendeleo gani hayoo.

Inawezekana vipi jamani uwezeshwe fedha za kwenda kajadili maendeleo ya watu wako halafu kesho usimame mbele kutuambia una nia ya dhati ya kukomboa kama wananchi wa Bara la Afrika.

Huku ni kudanganyana kwasababu katika mazingira ya kawaida tu asilimia 72 ya bajeti ya shughuli za AU inafadhiliwa na wafadhili wa kimataifa wanaoongozwa na Marekani na Umoja wa Ulaya, hapo unategemea nini.

Hivi kweli viongozi wa AU hawana aibu kwenye mioyo yao kwa jinsi walivyoweza kujitajirisha binafsi na familia zao na kusababisha AU kushindwa kuwa na uwezo wa kiuchumi wa kuwaita viongozi wake.

Nani hajui jinsi marais wa Afrika walivyo matajiri wa kutupwa wengine wakizizidi hata nchi zao kwa utajiri, nani hajui watoto wa marais wa Afrika walivyo Ma-Trilionea kutokana na kujichotea utajiri wa wananchi wote.

Kitu gani ni kigeni kwa rais wa nchi za Afrika anayeingia madarakani akiwa lofa wa kutupwa yeye na familia yake lakini pindi anapokaribia kuondoka kila ndugu na jamaa wa rais huwa amekwisha kutajirika na kuwa bilionea.

Si hivyo tu wapo marais wengine wao hunogewa na utamu wa madaraka ya urais na kuanza kuwaza kubadilisha Katiba ili tu wapate mwanya mwingine wa kuendelea kuiba mali za wananchi wanaowatawala.

Hivi nani hafahamu kwamba baadhi ya marais Afrika wapo wanaolipwa mshahara mkubwa zaidi kwa mwezi mmoja ambao haulingani na hali za maisha ya watu wanaowaongoza?

Sasa basi azimio la siku mbili la viongozi wa Afrika (AU) lililopendekeza kuanzishwe kodi ili kugharamia shughuli za umoja huo ikiwamo kufanikisha mikutano yao, kwa niaba ya wananchi wa Afrika nalipinga.

Huo ni mwendelezo wa kumnyonya Mbu damu huku kikundi cha wachache katika Afrika kikijenga uzio wa kuishi peponi wakati wananchi maskini wakifa kwa njaa na vita inayosababishwa na kukindi cha viongozi.

Azimio hilo limesema ili kuziba pengo la asilimia 72 wametafuta namna ya kujikwamua na utegemezi huo kwa kupendekeza kodi itozwe kwenye tiketi za ndege, hoteli na ujumbe mfupi wa simu za mkononi.

Chini ya Mwenyekiti wao Mzee, Rais Robert Mugabe viongozi hao wanasema mpango huo utaipatia AU Dola Milioni 730 kwa mwaka, huku nyongeza ya ujumbe mfupi wa simu ukitarajiwa kuzalisha Dola Bilioni 1.6.

Fedha hizo ni nyingi na zimeelekezwa kukatwa kutoka kwenye jasho la wananchi wa Bara la Afrika ambao hadi leo hii hawajaona umuhimu wala manufaa ya vikao vya wakubwa hao Addis Ababa.

Huu ni unyonyaji mwingine kwa wananchi dhidi ya viongozi hawa walioshindwa kuletea maendeleo Bara la Afrika, wameshindwa kulinda maisha ya watu, watu wao wanakufa kutokana, magonjwa na njaa.

Eti wamekutana kupanga mango dhalimu wa kunyonya maskini wawachangie ili wakakutane Adidis Ababa kula bata na wake zao na wafuasi wao.

Hatutakubali marais wa Afrika mnazo fedha kwenye akaunti zenu ndani na nje ya Afrika chukueni ili mkutane AU vikao ni vyenu si vya wananchi, vingekuwa vya wananchi tungeona vita, umaskini na njaa inaisha Afrika.

Mwisho.


No comments:

Post a Comment