NA ELIYA MBONEA, ARUSHA
MKUU wa Mkoa wa Arusha Daudi Ntibenda amewapiga marufuku
wafanyakazi wa Serikali mkoani hapa kufanya kazi za “umeneja” kwa wanasiasa
hasa nyakati za uchanguzi.
Agizo hilo alilitoa hivi karibuni kwenye hafla ya kuuaga
mwaka 2014 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2015 iinayoandaliwa kila mwaka na
Jeshi la Polisi mkoani hapa.
Katika hafla hiyo Ntibenda aliyekuwa mgeni rasmi alisema,
kwamba ni aibu kwa mfanyakazi wa Serikali kujihusisha au kuwa meneja wa
mwanasiasa wa chama fulani.
“Ni aibu kubwa kwa mtumishi wa serikali kuwa meneja wa mtu
wa kisiasa. Nawaagiza wafanyakazi wa serikali fanyeni kazi mlizoajiriwa
kuzifanya kwa maendeleo ya Watanzania.
“Nyinyi kazi yenu ni kupiga kura, suala la kufanya siasa
hili halipo kwenye ajira zenu. Mungu ndiye anayejua nani atakuwa kiongozi wetu
na hata kwenye ngazi za chini Mungu peke yake ndiye anajua,” alisema Ntibenda
Ntibenda aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Muhambwe
wilayani Kibondo mkoani Kigoma mwaka 2005 aliwataka watumishi hao kuwaachia
watu waliomo kwenye siasa kutekeleza wajibu wao.
“Tatizo la Arusha panaongoza sana kwa kuwa na siasa chafu,”
alisema RC Ntibenda.
Akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Arusha
alisema tayari wamekutana na kuangalia changamoto zinaoukabili mkoa huo ikiwa
ni pamoja na namna ya kuzitatua.
Alisema katika miaka mwili iliyopita Arusha ilikabiliwa na
hali tete ya usalama wa maisha ya wananchi pamoja na kutetereka kwa sekta ya
utalii kutokana na vitendo vya kurusha mabomu katika nyumba za ibada, starehe
na mikutano ya siasa.
“Nilipongeze utendaji wa jeshi la polisi kwa usimamizi wa
amani katika mkoa wa Arusha na hasa Jiji la Arusha. Wapo waliotaka kusiwe na
amani, lakini kuanzia uchaguzi mkuu wa serikali za mitaa tumeza kuufanya kwa
amani,” alisema Nitenda.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Liberatus
Sabas akizungumza katika hafla hiyo alisema kwamba waliweza kufanikiwa kukamata
na kurejesha hali ya amani katika jiji hilo kutokana na kila mtu kutimiza
wajibu wake.
“Hivyo basi kupitia hafla hii niwaombe wananchi wa Arusha
waendelee kutoa taarifa kwa jeshi la polisi kwani wao ndio wenye taarifa zaidi
za wahalifu kutokana na watu hao kuishi nao mitaani,” alisema RPC Sabas.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment