Wednesday, February 11, 2015

UMEME WA SOLAR WANUSURU MAISHA YA WAJAWAZITO, WATOTO


NA ELIYA MBONEA, ARUSHA

TEKNOLOJIA mpya ya Nishati mbadala ya umeme jua (Solar), imetajwa kuwa mkombozi kwa shughuli za kijamii ikiwamo kunusuru afya za watoto na wanawake wajawazito pindi wanaojifungua usiku kwenye vituo vya afya na zahanati maeneo ya vijijini.

Kutokana na umuhimu wa Nishati hiyo, Serikali na wadau wengine wameombwa kuendelea kuunga mkono teknolojia hiyo kwa kuhakikisha inawafikia wananchi ambao hawajafikiwa na umeme ukiwamo wa Solar.

Mwito huo ulitolewa jijini hapa na Diwani wa Kata ya Themi Melans Kinabo alipokuwa akizundua jengo jipya la Kampuni ya Solar ya Mobisol lilipo eneo la Njiro.
  
“Endapo teknolojia hii itaendelezwa na kuungwa mkono hakika serikali itakuwa imesaidia shughuli nyingi za kijamii hasa kwenye kuokoa maisha ya mtoto na mama wajawazito kwenye vituo vya afya na zanahati,” alisema Diwani Kinabo na kuongeza:

“Ipo haja kubwa kwa serikali na wadau kuziunga mkono teknolojia hizi mpya za umeme wa jua kwani kwa maeneo ambako zimeanzia kunaonekana kuwa na mafanikio makubwa hasa kwa kuibua shughuli za kiuchumi na kuongeza pato kwa wananchi wa kawaida,” alisema.

Kwa upande wake Msaidizi wa kitengo cha Masoko wa Mobisol, Bryson Kisamo alisema kuwapo kwa kampuni hiyo jijini Arusha kumesaidia kutoa ajira kwa vijana zaidi ya 150 .

“Vijana hawa hawakuwa na ajira kabisa hapo awali hivyo ujio wa Nishati mbadala umepunguza vijana kukaa vijiweni kwani hivi sasa wanajishughulisha katika kuitafuta wateja na kuuza vifaa mbalimbali,” alisema Kisamo.

Alisema idadi kubwa ya wananchi mkoani Arusha wamenufaika na mitambo ya sola ya Mobisol  kutokana na mfumo wa kununua kwa mkopo wa gharama nafuu na kisha kulipia kwa awamu kulingana na uwezo wa mteja.

Naye Mkazi wa Kwamrombo aliyenufaika umeme huo wa Solar,  Siasa Athuman alisema aliamua kuanza kutumia mitamo hiyo  kutokana na atha aliyokuwa akiipata ya kukatika umeme wa Grid ya Taifa mara kwa mara.

“Shughuli zangu zinanihitaji kuzifanyaa kwa saa 24 hivyo kukatika kwa umeme mara kwa mara kulikuwa kunaniingizia hasara ambayo sikuwa naitegemea,” alisema Athuman.

Mwisho.


No comments:

Post a Comment