Wednesday, February 11, 2015

POLISI ARUSHA WADAIWA KUMHUJUMU RC!

NA MWANDISHI WETU, ARUSHA.

BAADHI ya askari polisi wanaowamiliki wa daladala za biashara ya usafirishaji  abiria katika Jiji la Arusha wanadaiwa kuhujumu jitihada za Mkuu wa Mkoa wa Arusha Daudi Ntibenda za kuboresha huduma hiyo.

Taarifa za hujuma hizo alizitoa hivi karibuni mbele ya askari na familia zao pamoja na wadau mbalimbali  katika sherehe zilizoandaliwa na jeshi hilo  za kuaga mwaka 2014 na kuukaribisha mwaka 2015 zilizofanyika jijini hapa.

Miongoni mwa jitihada za kuboresha usafiri huo zilizofanyika mpaka sasa ni kubuni njia ‘ruti’ mpya zilizoanza kutumika, kuhamisha kituo cha daladala kilichokuwa katikati ya Jiji kwenda Ngarenaro-Samunge na kudhibiti msongamano wa magari usio wa lazima.

Ili kuleta ufanisi na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa agizo la Kamati ya Ulinzi na Usala ya mkoa ya kuhamisha kituo cha daladala na kuondoa msongamano, Ntibenda kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwamo Polisi aliagiza kazi hiyo kufanywa na kampuni binafsi ya Jacob Associate ya Arusha.

Uamuzi wa kutumia kampuni hiyo badala ya askari wa usalama barabarani ulifikiwa baada ya kubainika kuwa idadi kubwa na magari yanamilikiwa na askari hao hivyo kutokana na mgongano wa kimaslahi wasingeweza kusimamia kikamilifu uamuzi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.

Kutokana na kupata taarifa za  kuhujumiwa Ntibenda alitoa onyo kali kwa askari wanaomiliki daladala  kuwa kitendo cha kukatisha ‘ruti’ au kukataa kwenda Samunge ni kupima nguvu ya Serikali na kupuuza maagizo halali hivyo asilaumiwe kwa hatua atakazochukua.

“Nina orodha ya magari yanayokatisha ‘ruti’ gari hizi zinaipima nguvu Serikali ili waone ina nguvu kiasi gani, sasa nawaambia hatutasita kufutua leseni zao,” alisema Ntibenda na kuongeza:

“Kazi zangu zinakwenda kwa mtindo wa Katapila hivyo atakayelaza damu ntamzoa,” alionya.

Mwisho.

   

No comments:

Post a Comment