Wednesday, February 11, 2015

LOWASSA AZIDI KULIA GESI IBORESHE ELIMU

NA ELIYA MBONEA, ARUSHA

WAZIRI Mkuu wa zamani na Mbunge wa Jimbo la Monduli Edward Lowassa ameendelea kulia na uboreshwaji wa elimu nchini akisisitiza mapato yanayotokana na rasilimali ya gesi yaelekezwe katika kuinusuru sekta ya elimu.

Kauli hiyo aliitoa wakati wa ziara yake kibunge ya kutembelea Chuo cha Maendeleo ya Jamii (CDTI) na Chuo cha Ualimu Monduli jana ambapo alizungumza na wanafunzi wa vyuo hivyo ikiwa ni pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili.

Akizungumza na Jumuiya ya wanafunzi na walimu wa Taasisi hizo kwa nyakati tofauti Lowassa alisema, siku zote ataendelea kuwa mkereketwa wa elimu  kutokna na umuhimu wake katika maendeleo ya taifa.

“Mimi ni mkereketwa wa elimu, naamini ukimuwekea mtu elimu kichwani atakuwa na uwezo wa kufanya shughuli za maendeleo kwa upeo mpana, kama ni kulima, kufuga, biashara na shughuli zozote atatumia elimu yake,” alisema Lowassa na kuongeza:

“Sasa hivi tunachimba Gas na uwezekano wa kuwa nayo miaka mingi ijayo ni mkubwa. Inawezekana tukatumia mapato ya rasilimali ya Gas kuhakikisha elimu yetu inakuwa ya bure na bora au tukope mabilioni ya fedha ili tuwekeze kwenye elimu, hili linawezekana,” alisema.

Alisema elimu ya Tanzania inakabiliwa na changamoto ya ushindani katika soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki kutokana na nchi ya Kenya na Rwanda kuboresha mindombinu ya elimu nchini humo kwa kuongeza ushindani zaidi.

Lowassa alisema kwamba mipaka ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kamwe haikwepeki hasa katika suala la ajira hatua ambayo kama elimu ya Tanzania isipofanyiwa mageuzi makubwa uwezekano wa kuendelea kubakia nyuma kwenye soko la ajira utakuwa mkubwa.

“Nchi ya Rwanda walipata ofa ya kulekea wanafunzi karibia 300 nchini Marekani kusoma kila mwaka na hawa wakimaliza masomo wanarudi nchini mwao. Hebu fikirieni Kenya kuna wanafunzi wanaomaliza udaktari kwa mwaka takribani 5,000.

“Hawa wote mwisho wa siku lazima watataka kuingia kwenye soko la ajira la Afrika Mashariki, hawa watu unadhani wataenda wapi kutafuta soko lazima mwisho wa siku watajikuta wameingia nchini mwetu, ndio maana nasema elimu inahitaji kufanyiwa mageuzi makubwa,” aliema Lowassa.

Alisema wakati jitihada za kuboresha elimu zikifanyika kwa watalaamu na wadau wa elimu kuendelea kujadili na kutathimini namna ambavyo elimu hiyo itamtengenezea ajira kijana wa Kitanzania.

Akitolea mfano wa maeneo ambayo ni rahisi kumtengenezea ajira kijana wa Kitanzania aliyemaliza masomo  ni kwenye sekta ya kilimo ambacho kinaweza kuchukua vijana wengi kama ilivyo kwa nchi zilizoendelea ambazo ziliwawezesha wasomi kujiajiri kwenye kilimo.

“Niwapongeze sana Mkuu wa Mkoa wa Tabora Fatuma Mwassa na Mkuu wa wilaya ya Igunga Elibariki Kingu viongozi hawa wameweza kujenga mazingira ya kuwashawishi vijana kupenda kilimo, sasa tunahitaji viongpozi kufanya hivyo,” alisema Lowassa.

Mwisho.


No comments:

Post a Comment