Wednesday, February 11, 2015

MDAHALO EABMTI WAIBUA MAPYA ARUSHA


NA ELIYA MBONEA, ARUSHA

VYAMA vya siasa na wagombea nafasi za uongozi katika Uchaguzi Mkuu wametakiwa kutembelea wananchi ili wapate agenda zinazotokana mawazo yao badala ya viongozi kupanda jukwaani wakiwa na agenda mifukoni.

Hayo yalibainika jijini hapa juzi wakati wa Mdahalo wa kuamua vipaumbele vya Mkoa wa Arusha katika mijadala ya Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka huu ulioandaliwa na Taasisi ya Biashara, Habari na Mafunzo ya Afrika Mashariki (EABMT) kwa kushirikiana na Asasi ya Twaweza.

Mdahalo huo ulioongozwa na Mwenyekiti Mtendaji wa EABMT Rosemary Mwakitwange  ambapo ulitoa fursa kwa wananchi, serikali na wawakilishi kwa pamoja na kutambua changamoto zinazowakabili ili kuepuka kuwa wasindikizaji wa mijadala.

Wakizungumza katika mdahalo huo pamoja na mambo mengine wananchi hao walianisha mambo wanayotaka wao yazungumzwe au kuingizwa kwenye Sera za vyama vya siasa badala ya vyama na wagombea wao kuwafuata wakiwa na sera zao mifukoni.

Akichangia katika mdahalo huo mkazi wa Arusha Viola Lazaro alisema, umefika wakati wa kuwa na Sera na Ilani ya uchaguzi zinazotokana na maoni ya wananchi itakayowezesha kuwa na kitu kimoja cha kitaifa badala ya Ilani za kila chama.

“Tangu mwanzo tulikosea kama Taifa, kwani tulikuwa tunatengeneza Ilani na sera zetu kama vyama na wagombea. Na tunapokwenda kwa wananchi kuwaeleza kile tulichonacho tunajikuta wananchi wanahitaji vitu tofauti kabisa.

“Sasa nashauri tuwe na mazungumzo kwanza na wananchi watuambie wanataka nini, au wangependa kuwaona viongozi  wanaokwenda kuwaomba kura je watatimiza yale waliyoyasema wananchi wenyewe!,” alisisitiza Viola.

Kwa upande wake Prosper Mfinanga aliwataka viongozi watakaokwenda kwa wananchi kuwaomba kura wahakikishe wanajadili maisha ya wananchi badala ya kutoa ahadi hewa zisizotekelezeka kwa miaka mitano.

“Arusha tunahitaji kiongozi mbunifu si kiongozi anachaguliwa miaka mitano anaishia kujinufaisha na familia yake, wapo hapa tumewaona amechaguliwa akiwa hana kitu leo amenunua magari na kuhamia kwenye majumba makubwa,” alisema Mfinanga.

Hata hivyo baadhi ya wachangiaji katika mdahalo huo kwa nyakati tofauti walisisitiza baadhi ya mambo yanayohitajika katika jiji la Arusha kuwa ni amani hivyo viongozi watakao kwenda kwa wananchi wahakikishe wanatoa majibu sahihi ni kwa jinsi gani watairejesha amani iliyopotea jijini Arusha.

Kwa upande wake Mwenyekiti Mtendaji Mwakitwange alisema vipindi vya midahalo ya Tanzania Tuitakayo vitarushwa kupitia Televisheni za ITV na Star Tv ambapo hadi sasa tayari midagalo hiyo imekuwa na mchango mkubwa kwa vyombo vya habari, waandishi, watawala, wawakilishi na wananchi kwa ujumla.

“Kutokana na mafanikio hayo tumeona ni vyema zaidi kufanya mdahalo kwa ngazi ya mkoa ili kuhakikisha mambo wanayoyataka wana mfano wa Arusha na maeneo mengine, yanaingizwa kwenye mijadala ya kitaifa,” alisema Mwakitwange na kuongeza:

“Tumeratibu mdahalo huu kwa mara ya kwanza, uliohusisha wasemaji kutoka serikalini, vyama vya siasa, chama cha wafanyabiashara, asasi za kiraia, makundi maalumu na wananchi,” alisema.

Mwisho.  





No comments:

Post a Comment