NA ELIYA MBONEA, ARUSHA
MKUU wa Mkoa wa Arusha Daud Ntibenda amewatahadharisha
wafanyakazi wa umma na wananchi kuwa kazi zake anazifanya kwa mtindo wa
Katapila hivyo kwa atakayelaza damu asishangae kuzolewa.
Kauli hiyo aliitoa hivi karibuni jijini hapa alipozungumza
na wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama mkoa na wilaya, Maafisa, Wakaguzi na
askari wa Jeshi la polisi mkoani Arusha kwenye hafla ya kuuga na kuukaribisha
mwaka mpya 2015.
Akizungumza katika hafla hiyo alimshukuru Rais Jakaya
Kikwete kwa kumteua kusimamia Mkoa wa Arusha wenye changamoto nyingi, hivyo
aliliomba jeshi la polisi na vyombo vingine vya usalama ikiwamo jamii kumpa
ushirikiano wa kazi.
“Kazi zangu zinakwenda kwa mtindo wa Katapila kwa hiyo ni
waombe wafanyakazi na wananchi tusilaze damu tufanye kazi na majukumu tuliyokabidhiwa,
nje ya hapo mimi nitakuzoa,” alisema RC Ntibenda.
Alisema akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama
Mkoa wa Arusha tayari kwa kushirikiana na wajumbe wake wamekutana na kuangalia
changamoto mbalimbali zinaoukabili mjio huo ikiwa ni pamoja na namna ya
kuzitatua.
Alisema katika miaka mwili iliyopita Arusha ilikabiliwa na
hali tete ya usalama wa maisha ya wananchi ikiwa ni pamoja na kutetereka kwa
sekta ya utalii kutokana na vitendo vya kurusha mabomu katika nyumba za ibada,
starehe na mikutano ya siasa.
“Nilipongeze utendaji wa jeshi la polisi kwa usimamizi wa
amani katika mkoa wa Arusha na hasa Jiji la Arusha. Wapo waliotaka kusiwe na amani,
lakini kuanzia uchaguzi mkuu wa serikali za mitaa tumeza kuufanya kwa amani,”
alisema Nitenda.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Liberatus
Sabas akizungumza katika hafla hiyo alisema kwamba waliweza kufanikiwa kukamata
na kurejesha hali ya amani katika jiji hilo kutokana na kila mtu kutimiza
wajibu wake.
“Hivyo basi kupitia hafla hii niwaombe wananchi wa Arusha
waendelee kutoa taarifa kwa jeshi la polisi kwani wao ndio wenye taarifa zaidi
za wahalifu kutokana na watu hao kuishi nao mitaani,” alisema RPC Sabas.
Naye Afisa wa Polisi mkoani hapa SSP Mary Lugola akisoma
risala alisema, ni imani yao kwamba kuteuliwa kwake kuwa Mkuu wa mkoa
kutachochea mshikamano uliopo baina ya polisi na jamii na kuleta mafanikio
katika kipindi cha Mwaka huu.
No comments:
Post a Comment