JICHO LA ARUSHA
NANI asiyejua kwamba takribani miaka 10 iliyopita hali ya
kiusalama katika Mkoa wa Arusha na hasa
mitaa yake hali ilikuwa tete?
Arusha ilikabiliwa na mazingaombwe mengi, ukianzia ukanda
wilaya ya Ngorongoro, Longido unaopakana na nchi jirani ya Kenya hali ilikuwa
mbaya.
Pia ilikuwa hata ukiingia mitaa ya Jiji la Arusha na maeneo
jirani, usalama wa raia na mali zako ulikuwa mdogo kiasi cha kulazimisha wafanyabiashara
kufunga maduka yao mapema au kuwahi nyumbani mapema .
Kwa ujumla vitendo vya ujambazi wa kutumia silaha, iwe
bastola, bunduki za kivita na silaha za kijadi ulishika kasi kiasi na kuigeuza
Arusha kuwa eneo la kujifunzia uhalifu.
Katika ninachotaka kukizungumzia leo katika makala haya
sitaki kuonyesha kwamba sasa vitendo hivyo havipo tena au havifanyiki katika
mkoa wa Arusha, La hasha, ninachotaka kuzungumzia au kugusia ni kupungua kwa
vitendo hivyo tofauti na miaka 10 iliyopita.
Pengine twaweza kukubaliana kabisa kwamba Mwaka 2006 mara
baada ya kuteuliwa kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi mpya IGP Said Mwema akichukua
nafasi ya IGP Omar Mahita, hali ilianza
kubadilika, pole pole.
Ni wazi kwamba katika kipindi hicho ndipo tulipoanza kuona
maboresho ya Jeshi la Polisi nchini yakianza.
Katika utawala wa IGP Mstaafu Mwema tumeliona Jeshi la
Polisi nchini likianza kuchukua sura mpya ya kuwa karibu na wananchi wake kwa
kupitia mfumo wa Polisi Jamii au Shirikishi.
Mfumo huo umerejesha matumaini makubwa na imani kwa
wananchi juu ya ufanyakazi kazi wa askari polisi, lakini pia mfumo huo wa
Polisi Jamii umeweza kulisaidia kwa kiwango kikubwa jeshi hilo linapata taarifa
za ndani za kiuhalifu kutoka kwa wananchi.
Hali hii ni tofauti na zamani kwani wananchi waliowengi
waliogopa kutoa taarifa polisi, wakiamini taarifa za uhalifu watakazozitoa
zinaweza kuwarudia na kujikuta wakihatarisha maisha yao.
Vitendo hivyo kwa ujumla vilikuwa vimekithiri miongoni mwa
baadhi ya askari polisi wasio waaminifu, japo hata kwa sasa bado kuna virusi
vya aina hiyo vinaendelea kujionyesha kwa mbali.
Hata hivyo ni wazi kwamba ujio mpya wa IGP Ernest Mangu
unaonekana kuwa wenye manufaa katika juhudi za kuendelea kuliboresha jeshi la
polisi nchini, kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake IGP mstaafu Mwema.
Ni wazi kwamba maboresho yaliyoanzishwa na Mwema
yalisababishwa na vichocheo mbalimbali vikiwamo vya mabadiliko na kasi ya
uhalifu, hali ya mambo isiyoridhisha ndani ya jeshi hilo ikiwamo miundombinu,
vifaa na mifumo mzima.
Katika kuhakikisha maboresho yanaendelea kuzaa matunda
Jeshi la Polisi mkoani Arusha limekutana kwa pamoja na maofisa wa Polisi
wanaosimamia Polisi Jamii kuanzia ngazi ya Kata, Tarafa, wilaya, mkoa na Makao
Makuu, wakiwamo pia wadau ili kufanya tathimini ya kazi.
Katika tathimini hiyo yapo mengi ambayo kwa hali ya usalama
katika Mkoa na Jiji la Arusha yanaweza kutafsiriwa kama sehemu ya matunda ya
kuwapo kwa mfumo wa polisi Jamii ambao umeweza taarifa za mitaani na
vichochoroni kuwafikia askari polisi na kuzaa matunda.
Leo hii kila katika Jiji la Arusha na maeneo ya wilaya ya
Ngorongoro kumekuwa na mafanikio kwa jeshi la polisi kwa kushirikiana na polisi
jamii ambapo kwa nyakati tofauti wananchi wanaomiliki silaha zikiwamo za kivita
wamezikabidhi kwenye vyombo husika kwa amani.
Lakini si kwa Ngorongoro tuu, kwani hata matukio ya
milipuko ya mabomu iliyokuwa imeanza kushika kasi ya ajabu na kushindwa kuelewa
watu wa aina hii, walipata wapi nguvu na ujasiri wa kuendelea kutupa mabomu
kwenye mikusanyiko ya watu, nyumba za ibada ikiwamo kumwagia watu tindikali??
Kundi hili la watu wachache wanaokubali kutumika kuuwa
ndugu zao kwa malengo wanayoyajua wao, sasa limethibitiwa lote na vyombo vya
dola. Lakini inabainishwa kuwa chanzo cha mambo yote hayo ni uwapo wa mfumo wa
Polisi Jamii uliowezesha taarifa kuingia polisi na zisirudi mitaani kwa
wahusika.
Lakini pia vitendo hivyo tu kwani siku za hivi karibuni pia
jijini Arusha kuliibuka mauji ya wanawake wanaoendesha magari. Wamama hawa
walijikuta wakiwa kwenye wakati mgumu wa kushindwa kutembea kwa uhuru kisa tu
kuna watu wanaotishia kuwatoa roho zao.
Tayari mafanikio ya Polisi Jamii kwa kushirikiana na
watenda kazi wa polisi waliopata taarifa za kuwapo kwa mtu huyo nyumbani kwake,
zimezaa matunda kwani aliweza kushambuliwa na kuuawa.
Akiwa katika tathimini hiyo ya polisi jamii kama mgeni
rasmi Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magesa Mulongo anawashukuru sana askari polisi
waliopo kwenye Kata na Tarafa kwani
wameweza kufanya kazi nzuri iliyozaa matunda.
“Nimekuja kuwaambia mmefanya kazi nzuri sana. Kiburi chetu
chote na mafanikio yaliyoelezwa hapa bila uwakilishi wenu wa nguvu kwenye
maeneo ya kazi mliyopangiwa leo tusingefikia hapa tulipo, hongereni sana.
“Lakini pia wadau wa polisi jamii kutoka jamii
inayotuzunguka hakika niwapongeze kwa nzuri. Ukitazama historia aliyoisema
Kamanda kuhusu mawasiliano ya jeshi la polisi na wananchi hakika yalikuwa
yakuhisiana visivyo.
“Na mara nyingi raia ambao ndio wanaopaswa kutuletea
taarifa za mitaani mwao walishindwa kufanya hivyo, kwa madai kuwa wanaogopa
kutoa taarifa kwa jeshi la polisi kwasababu zitarudi tena kwao.
Kwa maelezo ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Liberatus
Sabas anasema amejiridhisha kwamba sasa mawasiliano kati ya wananchi na polisi
yamekuwa imara na yenye matokeo na mafanikio makubwa kupitia nyanja ya polisi
jamii.
Mulongo anasema ni wazi kuwa ukiangalia ukubwa wa Mkoa wa
Arusha na wilaya zake mfano Ngorogoro zina ugumu wa kutoka eneo moja kwenda
jingine.
“Lakini kama tumefikia mahali pa kupata taarifa ambazo
zimetuwezesha kupata mafanikio haya tuliyonayo leo kutoka kwa wananchi, lazima
tutembee kifua mbele.
“Nani asiyejua kama leo jambazi ukija Arusha lazima uangane
na nyonga yako, unaweza ukafanya lakini usitoke, na hata ukitoka hufiki mbali
na hata ukifika mbali tutakupata tu muda ukifika. Na hata wao wanajua kwasababu
matokeo yake wanayaona,” anasema Mulongo.
Mulongo anasema kuwa leo Taasisi yenye heshima ya Jeshi la
Polisi mkoani Arusha inafanya kazi na kupata mafanikio kutokana na kupata
taarifa kutoka kwa wananchi.
Na kazi hiyo imefanikiwa kwasababu ya askari polisi
waliotumwa kushirikiana na wananchi wanaendelea kutimiza wajibu wao.
“Jeshi la Polisi sasa mna taarifa kwasababu wananchi
wamejenga imani na jeshi la polisi, kwani ndani ya Polisi Jamii mrejesho
umekuwa mkubwa zaidi,” anasema Mulongo.
Kwa upande wake Kamanda Sabas akizungumzia mkutano huo
alisema, wamefanya tathimini hiyo kwa lengo la kujipima wapo wapi na wanaelekea
wapi ili waweze kuwa na utendaji kazi bora zaidi.
“Taasisi inayotaka mabadiliko ni vyema mambo wanayofanya
wakayafanyia tathimini, nasi tunasema huwezi kujifanyia tathimini mwenyewe.
“Lazima wawepo watu
watakao kuambia rekebisha hapa, ongeza hapa au punguza hapa na ndio maana raia
na wadau wengine wapo hapa kwenye mkutano wetu,” alisema Kamanda Sabas
Mwisho.
No comments:
Post a Comment