NA ELIYA MBONEA, ARUSHA
WAZIRI Mkuu wa zamani na Mbunge wa Jimbo la Monduli Edward
Lowassa ameendelea kulia na uboreshwaji wa elimu nchini akisisitiza mapato
yanayotokana na rasilimali ya gesi yaelekezwe katika kuinusuru sekta ya elimu.
Kauli hiyo aliitoa wakati wa ziara yake kibunge ya
kutembelea Chuo cha Maendeleo ya Jamii (CDTI) na Chuo cha Ualimu Monduli jana
ambapo alizungumza na wanafunzi wa vyuo hivyo ikiwa ni pamoja na kusikiliza
changamoto zinazowakabili.
Akizungumza na Jumuiya ya wanafunzi na walimu wa Taasisi
hizo kwa nyakati tofauti Lowassa alisema, siku zote ataendelea kuwa mkereketwa
wa elimu kutokna na umuhimu wake katika
maendeleo ya taifa.
“Mimi ni mkereketwa wa elimu, naamini ukimuwekea mtu elimu
kichwani atakuwa na uwezo wa kufanya shughuli za maendeleo kwa upeo mpana, kama
ni kulima, kufuga, biashara na shughuli zozote atatumia elimu yake,” alisema
Lowassa na kuongeza:
“Sasa hivi tunachimba Gas na uwezekano wa kuwa nayo miaka
mingi ijayo ni mkubwa. Inawezekana tukatumia mapato ya rasilimali ya Gas
kuhakikisha elimu yetu inakuwa ya bure na bora au tukope mabilioni ya fedha ili
tuwekeze kwenye elimu, hili linawezekana,” alisema.
Alisema elimu ya Tanzania inakabiliwa na changamoto ya
ushindani katika soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki kutokana na nchi ya Kenya
na Rwanda kuboresha mindombinu ya elimu nchini humo kwa kuongeza ushindani
zaidi.
Lowassa alisema kwamba mipaka ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki kamwe haikwepeki hasa katika suala la ajira hatua ambayo kama elimu
ya Tanzania isipofanyiwa mageuzi makubwa uwezekano wa kuendelea kubakia nyuma
kwenye soko la ajira utakuwa mkubwa.
“Nchi ya Rwanda walipata ofa ya kulekea wanafunzi karibia
300 nchini Marekani kusoma kila mwaka na hawa wakimaliza masomo wanarudi nchini
mwao. Hebu fikirieni Kenya kuna wanafunzi wanaomaliza udaktari kwa mwaka
takribani 5,000.
“Hawa wote mwisho wa siku lazima watataka kuingia kwenye
soko la ajira la Afrika Mashariki, hawa watu unadhani wataenda wapi kutafuta
soko lazima mwisho wa siku watajikuta wameingia nchini mwetu, ndio maana nasema
elimu inahitaji kufanyiwa mageuzi makubwa,” aliema Lowassa.
Alisema wakati jitihada za kuboresha elimu zikifanyika kwa
watalaamu na wadau wa elimu kuendelea kujadili na kutathimini namna ambavyo
elimu hiyo itamtengenezea ajira kijana wa Kitanzania.
Akitolea mfano wa maeneo ambayo ni rahisi kumtengenezea
ajira kijana wa Kitanzania aliyemaliza masomo ni kwenye sekta ya kilimo ambacho kinaweza
kuchukua vijana wengi kama ilivyo kwa nchi zilizoendelea ambazo ziliwawezesha
wasomi kujiajiri kwenye kilimo.
“Niwapongeze sana Mkuu wa Mkoa wa Tabora Fatuma Mwassa na
Mkuu wa wilaya ya Igunga Elibariki Kingu viongozi hawa wameweza kujenga
mazingira ya kuwashawishi vijana kupenda kilimo, sasa tunahitaji viongpozi
kufanya hivyo,” alisema Lowassa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment