JICHO LA ARUSHA
MPAKA ninapoandika makala haya, sijaamini macho yangu kama
picha iliyokuwa ukurasa wa mbele wa Gazeti kongwe na mahiri hapa nchini,gazeti la MTANZANIA ikimuonyesha msanii wa Bongo
Fleva Nassib Abdul “Diamond” akitumbuiza huku akiwa amevaa sare za Jeshi la Ulinzi
la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Niseme tu kwamba alichofanya Diamond ni dharau
iliyopitiliza dhidi ya hadhi na heshima iliyotukuka ya JWTZ.Kila ninapoiangalia picha hiyo
najiuliza maswali mengi sana ni kweli kwamba alikosa mavazi mengine ya kisanii??
Nani mshauri wa mavazi wa mwanamuziki huyo mpaka akaamua kugeuza sare za JWTZ kuwa
za kuchezea ngololo?
Mwanamuziki, msanii yeyote awe mdogo,mkubwa ana jina au
hana jina bado anabakia kuwa kioo cha jamii. Sasa kama Diamond amefikia mahali pa
kushindwa kuheshimu maagizo na amri zinazotolewa na vyombo vya Dola,
anawafundisha nini wengine au kizazi kijacho.
Kwa hakika elimu inayotolewa na mwanamuziki huyu na hasa
kwa vijana nchini ni kudharau maagizo, sheria na amri zinazotolewa na Taasisi
nyeti ikiwamo JWTZ.
Nasema ni dharau kwasababu taarifa za kukataza wananchi au
mtu yeyoye asiye askari na ambaye hakupitia mafunzo ya kijeshi kuvaa sare za
jeshi au zinazofanana na hizo zimekuwa zikitolewa na kurudiwa mara kwa mara.
Katika kuonyesha kuwa mtindo wa kuvaa sare za JWTZ umeshika
kasi pamoja na kuwapo makatazo mengi, Julai Mwaka huu JWTZ ilitoa taarifa kwa
vyombo vya habari ikipiga marufuku watu wanaovaa sare za majeshi kuacha mara moja vinginevyo wanakabiliwa na
adhabu kali.
Pamoja na katazo hilo, hivi karibuni kupitia Gazeti la
Mtanzania niliona picha ya askari wa JWTZ jijini Dar es Salaam akiwa anampigisha
mbizi kwenye dimbwi la maji kijana mmoja
aliyemkuta akiwa amevaa sare za jeshi hilo.
Sijui ni adhabu gani nyingine iliyofuata baada ya kumtaka
kijana huyo apige mbizi kwenye kijidimbwe kidogo cha maji mchana kweupee huku
akiwa amevua nguo zinazofafana na sare za jeshi na kubakia na kaptula yake.
Nikirejea kwenye dharau za Diamond ambaye nimeona picha
zake kwenye vyombo vya habari, ambapo Msemaji wa JWTZ Meja Joseph Masanja
alikiri kuanza uchunguzi wa wasanii Diamond na Nay wa Mitego ambao kwa pamoja
walivaa sare wakati wa onyesho la Fiesta jijini Dar es Salaam.
“Tumeanza uchunguzi wa kina kujua wasanii hawa wamepataje
nguo hizi, sheria za nchi haziruhusu mtu ambaye si askari kuvaa sare
hizi…nasema hilo ni kosa.
“Mtu yeyote atakayeonekana kuvaa nguo hizi, lazima vyombo
vya dola vimchukulie hatua, kwa msingi huo sisi kwa kushirikiana na polisi
tumeanza uchunguzi ili kubaini walipata wapi nani aliyehusika,” alisema Meja
Masanja.
Pengine nisirudie sana yaliyosemwa na Meja Masanja. Lakini
itoshe tu kusema kizazi cha Watanzania kilipofikia kipo kwenye uzao wa kambare
kuanzia baba, mama mtoto wote wanafuga ndevu ndani ya nyumba, kila mmoja ana
ndevu!
Hivi inawezekanaje katika hali ya kawaida matangazo
yatolewe kwenye vyombo vya habari kupiga marufuku. Lakini pia hazijapita wiki
mbili tangu kijana mwingine apewe suluba ya kupiga mbizi mchana kweupe Dar es
Salaam kwa kuvaa sare za JWTZ, kisha msanii anayeheshimika kwa baadhi ya
makundi kuamua kuonyesha dharau kwa JWTZ.
Kama nilivyosema nisiende sana huko kwa Meja Masanja,
lakini kuna mahali pananipa mashaka makubwa sana hasa uwezo wa Taasisi zetu
kuanzia Usalama wa Taifa, JWTZ yenyewe na hata Jeshi la Polisi.
Naamini kabisa Taasisi hizi nyeti za Serikali zipo mitaani,
ninaposema zipo mitaani namaanisha zimeajiri watu wanaoishi mitaani na
kushiriki kwenye aina zote za michanganyiko ya watu hapa nchini.
Sasa basi kila ninapoiangalia picha ya Diamond najiuliza
hivi ni kweli katika tamasha hilo Taasisi hizo nilizozitaja hapo juu na hasa
Usalama wa Taifa walishindwa kubaini mapema kuwa Diamond na Nay watapanda
jukwaa wakiwa wamevaa mavazi gani? Intelijensia iko wapi?
Na ni kweli kwamba katika viwanja vyote vile vya Leaders
hapakuwa na askari wa usalama wa taifa ambao wangeweza kutoa taarifa haraka kwa
maofisa wa JWTZ ili waje pale wamchukua Diamond na mwenzake?
Manake tumezeoa kuona vijana wasio kuwa na majina
wakipigishwa mbizi kwenye madimbwi ya maji kwa kuvaa sare zinazofanana na za
JWTZ.
Kwa dharau zilizoonyeshwa na Diamond na mwenzake Nay nina
tarajia kuona JWTZ likitoa fundisho kwao ili vijana na wasanii wengine waone kumbe huwa si
mzaha kuvaa sare za jeshi.
Ninachokiona mbele ya macho yangu kama mtashindwa au
kutanguliwa na huruma ya kuogopa majina ya wasanii hao, JWTZ mtakuwa mmetoa mwanya
kwa vijana wengine kuona kumbe hata wao wanaweza kuvaa endapo wakiwa na majina
makubwa kwenye sanaa.
Sipendi kupendekeza adhabu kwa dharau walizoonyesha, itoshe
tu kusema kwamba Watanzania tunatarajia kuona JWTZ likitoa onyo kali na la
mfano kwa wengine wanaopenda kuvaa sare za JWTZ na zinazofanana na hizo.
Si kwamba Diamond alikuwa hajui kama anafanya kosa alipoanza
kuvaa suruali, kombati, buti hadi kofia bali alifanya hivyo akijua anapima kina
cha maji ya JWTZ chini ya Mkuu wa Majeshi (CDF) Davis Mwamunyange kama ni
kirefu.
Nimesoma hoja za Makala ya Mwandishi Ester Mbussi. Nipenda
kumuambia katika hili tukubaliane kutokubaliana Diamond amefanya kosa na kosa lake
haliwezi kuhalalishwa kwa makosa yaliyofanywa na wengine.Tukifanya hivyo
itakuwa ni muendelezo wa kuruhusu uvunjifu wa sheria za nchi. Achukuliwe hatua
kali.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment