Wednesday, June 4, 2014

UPORAJI SEKTA ZA MBAO, UVUVI UNAZUIA AFRIKA KUENDELEA

RIPOTI  MAALUMU


RIPOTI mpya ya Jopo la Maendeleo ya Afrika ya 2014 imewahimiza viongozi wa Afrika kupambana na ukosefu wa usawa na kuitaka jamii ya ulimwengu kukabiliana na uporaji wa rasilimali za bara hili. 

Ripoti hiyo imezinduliwa nchini  Nigeria May 8 Mwaka huu na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Matifa Kofi Annan kwenye Mkutano wa Baraza la Kiuchumi la Ulimwengu kwa Afrika (World Economic Forum for Africa).

Kwa mujibu wa Africa Progress Panel (APP), ripoti hiyo imesema, rasilimali za Afrika zenye utajiri mwingi zinatoa nafasi ya kipekee ya ufanisi katika uimarishaji wa maisha ya raia wa Afrika.

Ripoti hiyo imewahimiza viongozi wa kisiasa wa Afrika kuchukua hatua sasa ili kupunguza ukosefu wa usawa kwa kuwekeza katika kilimo.
Pia, inataka hatua ya kimataifa kuchukuliwa ili kukomesha kile kinachotajwa kuwa uporaji wa sekta za mbao na uvuvi.

Annan anasema, baada ya zaidi ya mwongo mmoja wa ukuzi, kuna mengi ya kushangilia.

 “Lakini ni wakati wa kuuliza kwa nini ukuzi mkubwa wa jinsi hii haujasaidia hata kidogo kuwainua watu kutoka katika umasikini na kwa nini utajiri mwingi wa Afrika umeharibiwa kupitia mazoea ya ufisadi na uwekezaji usio mnyoofu.”

“Afrika ni bara lenye utajiri mwingi, kwa hivyo ni kwa nini fungu la Afrika katika utapiamlo ulimwenguni, na idadi ya vifo vya watoto inaongezeka haraka jinsi hii?

“Jibu ni kwamba ukosefu wa usawa unadhoofisha uhusiano kati ya ukuzi wa kiuchumi na maendeleo katika hali ya maisha ya watu,” anasema Annan.

Anasema, ingawa wastani wa mapato umeongezeka kwa theluthi moja katika mwongo uliopita, kuna Waafrika wengi zaidi sasa wanaoishi katika umasikini, takriban milioni 45  zaidi ya waliokuwapo katika mwisho wa miaka ya 1990.

Annan anasema malengo mapya ya kimaendeleo huenda yakajaribu kuodoa 
umasikini Afrika kufikia mwaka wa 2030, lakini kwa mkondo wa sasa,  Mwafrika mmoja kati ya watano bado atakuwa akiishi katika umasikini mwaka huo utakapofika.

Annan, ambaye aliathiri kwa kiwango kikubwa Malengo ya Maendeleo ya Milenia, anasema: “ Mbali na kuahidi kutimiza malengo makuu, nchi zinapojiunga na mfumo huu mpya wa kimaendeleo ulimwenguni zinapaswa kuahidi pia kupunguza mapengo yasiyoweza kutetewa katika bara hili, kati ya matajiri na masikini, maeneo ya vijijini na mijini, wanaume na wanawake.”

Anasema waandishi wa ripoti wanatambulisha kilimo kuwa msingi wa ukuzi ambao utapunguza umasikini. Wanadhihirisha kwamba masikini wengi wa Afrika wanaishi na kufanya kazi katika maeneo ya vijijini, na kwa wingi ni wakulima wadogo wadogo.

“Nchi ambazo zimejengwa juu ya misingi ya sekta bora za kilimo - kama vile Ethiopia na Rwanda  zimeonyesha kwamba maeneo ya vijijini yanaweza kuwa kichocheo kikubwa cha ukuzi wa pamoja na upunguzaji wa umasikini,” anasema Annan katika uzinduzi.

Anasema Ripoti hiyo imehimiza kuwe na “mageuzi ya kijani kibichi ya Kiafrika,” ambayo yanadondoa masomo kutoka kwa mageuzi ya Bara la Asia na kubadilishwa ili kufaa hali za Afrika.

Kwa wakati huu, gharama ya uingizaji wa chakula kutoka nchi za nje ni Dola za Marekani Bilioni 35, kwa sababu kilimo cha ndani kimekumbwa na uzalishaji wa kiwango cha chini, ukosefu wa uwekezaji, na ujitengaji wa kimaeneo.

 Annan anabainisha kwamba kuongezeka kwa uwekezaji katika miundombinu na utafiti kunaweza kuinua kwa kiwango kikubwa mavuno ya eneo hili na mapato ya wakulima.

Kwa wakati huo huo, kuondoa vikwazo vya kibiashara ndani ya Afrika kunaweza kufungua soko mpya.

Ingawa ripoti inakosoa viongozi wa Afrika, Ripoti ya 2014 ya Jopo la Maendeleo ya 
Afrika inaipa changamoto jamii ya kimataifa kuunga mkono jitihada za kimaendeleo za Afrika.

Inadhihirisha kwamba sekta za kilimo na mbao ndizo sekta mbili muhimu zinazohitaji kuimarishwa ili kupambana na uporaji wa rasilimali za asili.

Anasema uvuvi haramu, usiodhibitiwa na usioripotiwa umefikia kiwango cha juu kupindukia katika maji ya pwani ya Afrika. Afrika Magharibi hupoteza takriban Dola za Marekani Bilioni 1.3 kila mwaka.

Anasema zaidi ya gharama za kifedha, uporaji huo huangamiza jamii za kivuvi 
ambazo hupoteza nafasi muhimu za uvuvi, utayarishaji na uuzaji wa samaki. Dola nyingine Bilioni 17 hupotezwa kupitia ukataji haramu wa miti.

“Uporaji wa rasilimali ni wizi uliopangwa na unaofichwa kwa hila katika biashara. Meli za biashara za uvuvi za kigeni, ambazo husajiliwa katika nchi za Kiafrika kwa hila.

“Nna kupakua samaki katika bandari ambazo hazirekodi mapato yao, hazina maadiliambapo shughuli hizi haramu hukuza tatizo la ukwepaji wa kodi na kampuni bandia,”anasema Annan.

 Ripoti ya 2014 ya Jopo la Maendeleo ya Afrika imehimiza kuwapo kwa usimamizi wenye wahusika wengi wa sekta ya uvuvi ambao utatekeleza vikwazo juu ya meli ambazo hazisajili na kuripoti mapato yao

Aidha Ripoti hiyo imehimiza serikali ulimwenguni pote kuidhinisha Makubaliano ya Port State Measures, mkataba ambao unalenga kuzuia waporaji kupakua mapato yao haramu katika bandari.

Anasema viongozi wa kisiasa wa Afrika wameshindwa kusimamia rasilimali za asili kwa masilahi ya wanaozimiliki kihalisi  watu wa Afrika.

Anasema pamoja na kupoteza pesa kupitia uporaji na usimamizi mbaya wa kifedha, Waafrika wanapoteza pesa za kigeni, si ambapo wafadhili wanapokosa kuweka hadi zao tu, bali pia wakati Waafrika wanaoishi katika nchi za kigeni wanapotuma pesa kwa familia zao.

Inakadiriwa kwamba kila mwaka Bara hupoteza zaidi ya Dola za Marekani Bilioni 1.85 katika ada za kupindikia zinazotozwa kwa huduma hizo.

Annan anasema kutoka kwenye ripoti hiyo kwamba Serikali za Afrika sasa zina nafasi ya kutengeneza mifumo bora ya kodi  na kutumia pesa za umma vizuri kwa njia ya usawa.

Kwa mfano, asilimia 3 ya pato la jumla la eneo (GDP) kwa sasa huelekezwa kwa ruzuku za nishati ambazo kwa sehemu kubwa huenda kwa watu wa tabaka la kati kati.

Pesa hizo zinapaswa kugeuzwa na kupelekwa kwa matumizi ya jamii ili kuwapa masikini nafasi bora ya kutoroka mtego wa umasikini.

“Uwezo wa Afrika wa kukabiliana na hali ngumu, na ubunifu ni mkubwa. Tuna idadi kubwa ya vijana wenye nguvu. Wajasiriamali wetu wanatumia teknolojia kubadilisha maisha ya watu. 

“Tuna rasilimali za kutosha kulisha si sisi tu bali na  maeneo mengine pia. Ni wakati kwa viongozi wa Afrika na wawekezaji shirika wenye uwajibikaji kuibua uwezekano huu mkubwa,” anasema Annan.”

 Mwisho.



No comments:

Post a Comment