Wednesday, February 20, 2013

ASKOFU KATOLIKI AVILIPUA VYOMBO VYA ULINZI, USALAMA

KANISA Katoliki Jimbo Kuu la Arusha limeshangazwa na kitendo cha vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi kushindwa kuguswa na matukio ya mauaji na uchomaji wa makanisa nchini.

Tamko hilo lilitolewa juzi  na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha , Mhashamu Josephat Luis  Lebulu kwenye Ibada maalumu  ya kumuombea marehemu Padri Evarist Mushi wa Parokia ya Jimbo Kuu la Zanzibar aliyepigwa risasi Jumapili Februari17, Mwaka huu huko Visiwani.

Akizungumza kwenye mahubiri ya Ibada hiyo  iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Theresia  mjini Arusha  Askofu Leburu alisema, kuendele kujitokeza kwa matukio hayo ni dalili ya vyombo vya usalama kushindwa kazi yao.

“Wanaohusika na usalama wa watu pengine wanajua chanzo cha mauaji haya kiko wapi. Hivi inakuwaje vyombo vya ulinzi na usalama visiguswe na mauaji na uchomaji wa makanisa?”.

“Tukio la kupigwa risasi Padri Mushi limekuwa ujumbe mzito katika kipindi hiki cha Kwaresima, huu ni ujumbe maalumu wa Kristo Yesu”.

“Badala ya kulipuka na kutaka kulipiza kisasi, tumuombe Mungu awasamehe kwani hawajui walilolitenda,alisema Askofu Lebulu”

Akionekana kuchukizwa na uzembe huo wa vyombo vya dola kwa kushindwa kwao kubaini mapema dalili za kutishiwa kwa viongozi wa dini kwa kile alichosema kuwa kuna kanda ,cd,na vipeperushi vilikuwa vikisambazwa na taarifa zilishatolewa lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

“Uwezo wa kulipiza kisasi tunao  na sababu tungekuwa tunazo lakini Kristo Yesu ametutaka tusilipe kisasi, kwani kisasi ni chake , mafundisho yake ni tusilipe ovu kwa ovu .Tuwasamehe kwani hawajui watendalo “alisema na kuonya kuwa .

“Lakini katika mazingira haya hakuna binadamu anayeweza kunyamaza endapo hali ya mauaji ya viongozi wa dini na uchomaji wa makanisa ikiendelea,” alisema Askofu Lebulu.

Katika Ibada hiyo Askofu huyo aliwaomba waumini kuwaombea viongozi wa taifa wafumbuliwa macho ili waone vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na baadhi ya watu bila kuchukuliwa hatua.

“Mungu aguse hawa viongozi inakuwaje kwao kuwa ngumu kuona matusi na CD zinazohamasisha vurugu? Huu ni ujinga”.

Mhashamu Lebulu huku akifundisha kwa mifano ,alieleza kuwa serikali haipaswi kutazama tu vitendo vya vitisho kwa wananchi kwani ni kinyume cha katiba waliyoapa kuilinda .

“Serikali ni kama kinyonga ambaye ni rafiki wa tembo ambaye anakaribishwa kwa kinyonga lakini akawa anawauwa watoto wa kinyonga kwa kuwakanyaga bila baba kinyonga kuchukua hatua zaidi ya kumridhisha mkewe kwamba amemwangalia tembo kwa kuyazungusha macho yake”

“Pamoja na Tembo kuendelea kukanyanga watoto wale Kinyonga aliendelea kukaa kimya, hata hivyo alipoulizwa kulikoni akajibu hauoni jinsi nilivyomgeuzia macho yangu kila upande kwa kumwangalia?,” alisema Askofu Lebulu na kuwaacha waumini kuangua kicheko Kanisa humo.

Katika Ibada hiyo maalumu Askofu Lebulu alitangaza kuwa sadaka yote iliyotolewa itawasilishwa kama sehemu ya rambirambi Kanisa Kuu Zanzibar.

Padri Mushi alizikwa kwenye makaburi maalumu ya viongozi wa dini ya Kikristo yaliyopo eneo la Kitope Unguja.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment