Balozi wa Tanzania
nchini Ubeligiji, Dk. Diodorus Kamala ameteuliwa na mabalozi wa nchi za
Africa wanaoziwakilisha nchi zao nchini humo kuwa Mwenyekiti wao.
Balozi Kamala amepokea
uenyekiti huo kutoka kwa Balozi wa Swaziland nchini Ubeligiji, Joel
Nheleko aliyemaliza muda wake. Tanzania itashikilia kiti hicho kwa muda
wa miezi sita hadi Julai 1, 2013.
“Nimefurahi kupewa
heshima hii, na naamini nitaitumia fursa hii kufahamiana vizuri na
mabalozi wenzangu na kuvutia fursa za kiuchumi kwa nchi yetu,” alisema
Balozi Kamala.
Wakati huo huo,
juzi mabalozi wa nchi tano zinazozunguka Bonde la Ziwa Tanganyika,
walimchagua Balozi Kamala kuwa mwenyekiti wao.
Nchi wanachama wa Bonde la Ziwa Tanganyika ni Burundi, Rwanda, Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Zambia.
Nchi
hizi zimeunganisha nguvu kutafuta wafadhili kwa ajili ya maendeleo ya
Bonde la Ziwa Tanganyika, ambapo eneo la bonde hili lenye wakazi wastani
wa milioni 40 wanalenga kuliendeleza kwa ajili ya kujenga miundombinu, kurahisisha usafiri na usafirishaji, kujenga reli mpya na kuendeleza utalii.
Chini ya mpango huu
wanalenga pia kuboresha viwanja vya ndege vya nchi wanachama vya Mbala,
Kalemie, Bujumbura, Kigoma na Kasanga kwa nia ya kurahisisha usafiri wa
anga katika ukanda huu.
Dk. Kamala amekabidhiwa
jukumu la kuratibu mpango huu na kwa pamoja watatafuta fedha kutoka kwa
wafadhili kwa ajili ya mradi huu.
No comments:
Post a Comment