KANISA Anglikana Tanzania, limemchagua Askofu Mkuu mpya wa
Kanisa hilo, Dk Jacob Erasto Chimeledya (56), kuongoza kanisa hilo katika
kipindi cha miaka mitano.
Chimeledya ambaye amekuwa ni askofu wa sita amechukua nafasi ya
Askofu Valentino Mokiwa ambaye amemaliza muda wake kwa mujibu wa katiba ya
kanisa hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Dodoma jana, Katibu
Mkuu wa kanisa hilo, Dk Dickson Chilongani alisema uchaguzi wa askofu huyo
ulifanyika jana Katika Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika.
Alisema mkutano uliomchagua askofu huyo ulihudhuriwa na wajumbe
129 kati ya wajumbe 140 kati yao wakiwemo maaskofu 25 kutoka dayosisi
mbalimbali hapa nchini.
“Kwa kawaida katika uchaguzi askofu yeyote mwenye umri chini
ya 60 huwa ni mgombea hivyo katika uchaguzi huo maaskofu 21 walikuwa na sifa za
kugombea,” alisema.
Alisema kabla ya Dk Chimeledya kuchaguliwa kushika wadhifa
huo alikuwa ni askafu wa Dayosisi ya Mpwapwa.
Akielezea historia yake, Katibu huyo alisema Askofu Dk Chimeledya
alizaliwa mwaka 1957 na baada ya
kumaliza elimu ya sekondari alichukua stashahada ya Theolojia katika Chuo cha
St Philipo Kongwa.
“Baadae akaenda Kenya kuchukua shahada ya Divinity katika
chuo cha St Paul kabla ya kwenda kusomea shahada ya uzamili katika theolojia
nchini Marekani ambayo alimaliza mwaka 2003 na baada ya kuetuliwa kuwa askofu
alipewa shahada ya falsafa ya heshima,” alisema.
Alisema mwaka 2007 Dk Chimeledya aliteuliwa kuwa askofu
mwandamizi wa Jimbo la Mpwapwa chini askofu Simon Chiwanga.
Alisema baada ya Askofu Chiwanga kustaafu ndipo Dk Chimeledya
alipoteuliwa kuwa askofu wa Dayosisi hiyo ya Mpwapwa mwaka 2007.
Alisema askofu huyo mpya natarajiwa kuwekwa wakfu mwisho mwa
May mwaka huu Mjini Dodoma
Mwisho..
No comments:
Post a Comment