Thursday, March 1, 2018

BILIONI 4.5 ZAFANIKISHA KUKAMATWA MAJANGILI 2,617


Na MWANDISHI WETU
-ARUSHA

Watuhumiwa wa Ujangili  2,617 wamekamatwa kuanzia mwaka 2013 hadi 2015 katika maeneo ya mapori ya akiba ,mapori tengefu na hifadhi za jamii(WMA) ambayo kampuni sita zilizo chini ni mfuko wa kusaidia uhifadhi wa Friedkin(FCF) zimewekeza, huku zaidi ya sh 4.5 bilioni zikitumika katika vita dhidi ya ujangili.
baadhi ya watuhumiwa wa ujangili

Watuhumiwa hao wamekamatwa, kwa ushirikiano  pia na maafisa wa  Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori (TAWA) ambao kisheria ndio wanasimamia maeneo hayo .


Akizungumza na mwananchi,Meneja miradi wa FCF ,Nana Gross Woodley alisema watuhumiwa hao wa ujangili walikamatwa  katika maeneo  sita yenye zaidi ya ekari 2.8 milioni ambayo kampuni zilizo chini ya mfuko huo,zinafanya kazi za uwindaji wa kitalii, utalii wa picha na uhifadhi.

Kampuni hizo ni Tanzania Game Tracker Safari, Wenget Windrose Safari na Mwiba Holdings.

Maeneo ambayo kampuni hizo, zimewekeza ni  Pori la akiba la Maswa, maeneo ya Mbono na Kimali,eneo la Mwiba Ranchi na hifadhi ya jamii ya Makao, wilayani Meatu, eneo la Uvinza,Pori la akiba ya Ugala kusini na kaskazini, pori la akiba ya Moyowosi eneo la kusini na pori tengefu la ziwa Natroni.

Woodley  alisema, katika kipindi cha miaka mitatu, kila mwaka FCF imekuwa ikitumia kati ya sh 1.4 bilioni hadi 1.7 bilioni, katika vita dhidi ya ujangili, ikiwepo kununua magari,kuajiri askari ulinzi,kununua vifaa vya ulinzi na kuendesha operesheni mbali mbali dhidi ya ujangili.

Alisema kutokana na jitihada za FCF, kwa kushirikiana na TAWA na vyombo mbali mbali vya ulinzi na usalama, matukio ya ujangili yamepungua  kutoka  matukio 1226 mwaka 2013 hadi kufikia matukio 721 mwaka 2015.
Akitoa mchanganuo  wa majangili waliokamatwa katika kipindi cha miaka mitatu, alisema majangili wa nyama kwa ajili ya chakula waliokamatwa ni 304, majangili wa tembo, 18,majangili wa mbao 283, majangili wa urinaji asali 6 na majangili ya uvuvi haramu 142.

"katika kipindi hiki cha miaka mitatu 2013 hadi 2015, tumekamata wafugaji waliongia mifugo hifadhini,853,wajangili waliokuwa wakichoma mikaa 82, waliokuwa wameingia hifadhini kinyume cha sheria 881,walioingia kuchoma moto hifadhini 49"alisema

Mkurugenzi wa Mamlaka ya usimamizi wanyamapori(TAWA),Dk James Wakibara, ambaye mamlaka yake ndio inasimamia maeneo yote uhifadhi nje ya hifadhi za Taifa, akizungumza na mwananchi hivi karibuni alisema, jitihada za serikali na wadau mbali mbali ikiwepo wawekezaji wameweza kupunguza sana matukio ya ujangili.


Alisema kila mawaka matukio ya ujangili yamekuwa yakipungua hasa ujangili wa Tembo ambao unatoweka kabisa kutokana na ulinzi katika maeneo ya hifadhi na nje kuimarishwa.

Hata hivyo, alisema changamoto kubwa sasa katika uhifadhi ni tatizo la ongezeko la mifugo katika maeneo yaliyohifadhiwa.

"TAWA kwa kushirikiana na wadau wengine, tuna mikakati mbali mbali ya kukabiliana na matukio yote ya ujangili na kiasi kikubwa imefanikiwa lakini wito ni kwa wananchi wanaoishi jirani na hifadhi ni kuwa mabalozi wa kupinga matukio ya ujangili"alisema.

Mwenyekiti wa kijiji cha Makao, Anthony Philip ambapo kampuni a Mwiba holdings, imewekeza, alisema katika kijiji chake, kutokana na ushirikiano na wawezaji ambao wamefanikiwa kuwa na vikosi maalum vya kupambana na ujangili vya vijiji, wamedhibiti ujangili.

No comments:

Post a Comment