Thursday, March 29, 2018

AGPAHI YAKABIDHI MASHINE ZA KUCHUNGUZA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI,KOMPYUTA MKOA WA MWANZA



Shirika la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) limekabidhi mashine tano za kuchunguza saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake ‘cryotherapy machines’ mkoa wa Mwanza. 

Msaada huo umetolewa Jumanne Machi 27,2018 katika ukumbi wa mikutano waGOLD CREST HOTEL jijini Mwanza wakati wa kikao cha wadau wanaohusika katika mapambano ya VVU na Ukimwi mkoani Mwanza kwa ajili ya kupanga mipango na mikakati ya kupambana na VVU na Ukimwi. 

Akizungumza wakati wa kukabidhi mashine hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa alisema mashine hizo ni kwa ajili ya vituo vya afya vya Katunguru na Kabila vilivyopo wilaya ya Sengerema, hospitali ya Ngudu iliyopo wilayani Kwimba na zahanati ya Kirumba na kituo cha afya cha Buzuruga vilivyopo wilayani Ilemela. 

Dk. Sekela alisema mashine hizo tano zenye thamani ya shilingi milioni 6.8 zitatumika kutolea tiba mgando kwa akina mama wanaokutwa na dalili za mwanzo za kansa ya uzazi. “Mbali na shirika letu kuendelea kuboresha huduma za kinga na matunzo pia tunatoa huduma ya uchunguzi wa dalili saratani ya mlango wa kizazi kwa akina mama”,alieleza. 

Alisema huduma hiyo hutolewa katika vituo vya kutolea huduma ya afya 20 katika mkoa wa Mwanza. Dk. Sekela alisema shirika hilo mpaka sasa limetoa msaada wa ‘cryotherapy machines’ 17 katika mikoa sita ambayo ni Mwanza,Shinyanga,Tanga,Geita,Simiyu na Mara zote zikiwa na thamani ya jumla ya shilingi milioni 115.6. 

Dk. Sekela pia alikabidhi kompyuta 18 zitakazotumika kuhifadhi takwimu za wateja wa CTC katika vituo vya afya husika na kusaidia upatikanaji wa taarifa kwa haraka na kwa usahihi Zaidi mkoani Mwanza. “Tangu tuanze mradi wa Boresha, tutakuwa tumetoa jumla ya kompyuta 82 kwa mkoa wa Mwanza ambazo zinatumika kutunza taarifa za watu wenye VVU na Ukimwi”,alisema. 

Akizungumza kwa niaba ya wilaya zilizopokea mashine hizo,Mkuu wa wilaya ya Sengerema Emmanuel Kipole alilishukuru shirika la AGPAHI kwa kutoa msaada huo na kwamba watatumia vifaa vilivyotolewa kwa malengo yaliyokusudiwa. Awali akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella aliwataka wadau wote kuungana na kushirikiana ili kuhakikisha kuwa maambukizi ya VVU mkoa huo ambayo sasa ni asilimia 7.2 yanapungua. 

AGPAHI ni shirika la Kitanzania linalofanya kazi kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania kutoa huduma za afya hususani watu wanaoishi na Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi kwa fadhili wa Watu wa Marekani kupitia Centres for Disease Control (CDC). 
Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella akizungumza katika kikao cha wadau wanaohusika katika mapambano ya VVU na Ukimwi mkoani Mwanza kabla ya makabidhiano ya kompyuta na mashine tano za kuchunguza saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake ‘cryotherapy machines’.- Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog 
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa akielezea namna shirika hilo linavyotoa huduma ya kuwapima saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake. 
Dk. Sekela akizungumza na wadau wa afya mkoani Mwanza. 
Maboksi yenye kompyuta na mashine za kuchunguza saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake ‘cryotherapy machines’ zilizotolewa na shirika la AGPAHI kwa ajili ya vituo vya afya mkoani Mwanza. 
Kulia ni Dk. Mwakyusa akiwa ameshikilia moja ya mashine inayotumika kuchunguza saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake ‘cryotherapy machines’. 
Dk. Sekela akizungumza ukumbini. 
Katikati ni Dk. Sekela Mwakyusa akikabidhi mashine kwa Mkuu wa mkoa wa Mwanza,John Mongella (wa pili kushoto) na viongozi wa wilaya ya Sengerema. 
Zoezi la makabidhiano likiendelea. Wa kwanza kushoto ni Mwakilishi wa CDC nchini, Dk. Eva Matiko. 
Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Nyamagana, Mary Tesha akipokea cryotherapy machine. 
Mkuu wa wilaya ya Sengerema Emmanuel Kipole akitoa neno la shukrani baada ya makabidhiano ya mashine tano za kuchunguza saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake na kompyuta 18 zilizotolewa na shirika la AGPAHI. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

No comments:

Post a Comment