Baadhi ya nyumba za askari magereza zilizojengwa kutokana na faida iliyopatikana kupitia Shirika la Magereza Gereza Kuu Arusha.
-ARUSHA
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ameziagiza
Idara zilizopo wizarani kwake kufanya kazi za uzalishaji ili kuipunguzia mzigo
Serikali Kuu kwani kuendelea kutumia fedha za walipa kodi kutunza wahalifu
magerezani ni hasara kwa taifa .
Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa uzunduzi wa nyumba tano za
askari wa Gereza Kuu Arusha lililopo Kisongo mjini hapa zenye thamani ya Sh.
Milioni 253.9 zilizotokana na faida kutoka kwenye mradi wa kilimo unaofanywa na
Shirika la Magereza.
Akizungumza kwenye hafla Mwigulu alilishauri Jeshi la Magereza
nchini kuangalia uwezekano wa kuajiri kwa mikataba baadhi
ya wafungwa wenye vipaji waliomaliza vifungo vyao na waliorekebishika tabia ili
kuongeza nguvu kazi ya uzalishaji.
“Taasisi zilizobakia kuwa na maeneo mazuri ya uzalishaji ni
Magereza, bado yana fursa ya maeneo hayo kwenda kwenye mali. Tukizalisha kwenye
kilimo tunaweza kukipeleka kwenye matumizi mengine kama walivyofanya Arusha
wametoka kwenye kilimo kwenda kwenye nyumba.
“Hii itakuwa chachu kwa Taasisi zilizopo wizarani kwangu,
zifanye kazi ya uzalishaji kama huu ni ubunifu mzuri utakaowezesha kupunguza
mzigo kwa serikali ikiwamo kuzalisha chakula kwani ni hasara kutumia fedha za
walipa kodi kutunza wahalifu magerezani,” alisema Waziri Mwigulu.
Alisema ili kufikia malengo ya uzalishaji huo alishauri kwa
upande wa magereza kuangalia uwezekano wa watu wenye vipaji wanaomaliza adhabu
zao na kuonekana wamejirebisha hivyo watumike kuendeleza vipaji hivyo katika
uzalishaji.
“Magereza tunayo nguvu kazi ya kupunguza gharama ya uzalishaji,
Nchi yeyote inayoendelea huanza na viwanda vinavyotumia nguvu kazi ili watu
wapate ajira, sisi tuna fursa ya nguvu kazi na fursa ya kuwaendeleza hao
watu.
“Si wote, kuna watu wana vipaji na inatokea wanakuwa na makosa sasa
inapotokea wamemaliza adhabu zao na wanaonekana kujirekebisha na hawajui
wakitoka wataanzia wapi ni vyema mkaangalia utaratibu hata kama ni kwa mikataba
mifupi ya kuendeleza chini ya uangalizi wenu kwa lengo la nguvu kazi ya
kuzalisha zaidi,” alisema Mwigulu.
Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Dk. Juma
Malewa alimwambia Waziri Mwigulu katika uzinduzi huo kwamba tatizo la
makazi kwa Maofisa na askari wa Magereza kwa nchini nzima bado ni kubwa.
“Nyumba tulizonazo kwa nchi nzima ni 4,221 kuna upungufu wa
nyumba 9,800. Niishukuru Serikali kwani mwaka jana ilitoa Sh. Bilioni 10 kwa
ajili ya ujenzi wa nyumba za maafisa na askari 320 Gereza la Ukonga Dar es
Salaam,” alisema Kamishna Jenerali Dk. Malewa na kuongeza:
“Kwa upande wa ujenzi wa nyumba hizi tano hapa Arusha umefanywa
na mafundi wetu kwa maana ya askari na wafungwa kama sehemu ya kuwafundisha kwa
kutumia mafundi wa magereza ambapo wameweza kupunguza gharama za ujenzi kwa
asilimia 50,” alisema.
Naye Mkuu wa Magereza Mkoa wa Arusha Hamis Nkubas alisema mkoa
huo una upungufu mkubwa wa makazi ya askari ambapo nyumba zilizopo ni 142 na
hivyo kusababisha askari na maofisa 209 kutokuwa na makazi.
Nkubas alisema nyumba hizo tano zimejengwa Sh. Milioni 50. 7
kila moja na hivyo kufanya jumla ya Sh. Milioni 253.9 ikiwa ni gharama pungufu
kulingana na hali halisi kutokana na kutumia nguvu kazi na wataalamu ambao ni
askari na wafungwa.
“Iwapo nyumba hizi zingejengwa kwa kutumia mkandarasi gharama ya
nymba moja ingeongezeka kati ya asilimia 40 hadi 60 ya kiwango tulichotumia,”
alisema Nkubas.
Aidha Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema
aliishauri serikali kuweka mkakati wa kupata taarifa nyingi ndani ya magereza
ikiwamo kuwalinda watoa taarifa hizo.
“Ndani ya Magereza kuna taarifa nyingi kuliko nje kama
kukitengenezwa mkakati mzuri mnaweza kupata taarifa nyingi zaidi za kulisaidia
Taifa kuliko nje.Kwa uzoefu wangu ndani kuna taarifa nyingi,” alisema Lema.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment