Tuesday, November 22, 2016

PRECISION AIR YATUA HIFADHI YA SERENGETI

Na ELIYA MBONEA

-ARUSHA 

NDEGE ya Shirika la Precision Air imeanza safari za ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti iliyopo mkoani Mara ikilenga kukuza utalii na kurahisisha usafiri kwa watalii wa ndani na nje wanaotembelea vivutio nchini.

Ikiwa na uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 40 ndege hiyo iliwasili uwanja mdogo wa  ndege wa Seronera ndani ya Hifadhi hiyo jana huku ikiwa imebeba watali na baadhi ya abiria kutoka Dar es Salaam na Zanzibar walioelekea hifadhini.

Akizungumzia hatua hiyo inayotajwa kuongeza ufanisi katika sekta ya utalii nchini Meneja Uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Pascal Shelutete alisema, kuanzishwa kwa safari hiyo kutaongeza na kukuza idadi ya watalii.

Alisema kwamba, safari hizo za ndege ya moja kwa moja kutoka Dar es Salaam  kutaongeza ufanisi zaidi katika kukabiliana na changamoto ya miundombinu iliyokuwa ikizuia idadi kubwa ya wageni kutembelea  vivutio hivyo na kujikuta wengi wao wakiahirisha au kutumia muda mrefu.

 Alisema kwa kipindi kirefu TANAPA imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuyavutia mashirika ya ndege nchini kutengeza safari kwenye hifadhi zilizopo kwa lengo la kupunguza gharama na muda kwa watalii.

“Juhudi hizi zimezaa matunda sasa, tunatarajia kuendelea kufanya mazungumzo na mashirika mengine yakiwamo ATCL na Fast Jet nao waanzishe safari za moja kwa moja ndani ya hifadhi,”alisema Shelutete

Shelutete aliendelea kueleza kwamba, licha ya hifadhi zilizopo Ukanda wa mikoa ya Kusini za Katavi na Ruaha kuwa na viwanja vizuri vya ndege na vivutio vingi bado vimeendelea kuwa na idadi ndogo ya watalii hivyo aliwaomba wadau wa sekta ya usafiri anga kutumia fursa hizo.

Kwa upande wake Rubani wa Ndege ya Precision Air iliyowasili hifadhi hapo ikiwa na abiria, Benjamini Maluli alisema, hatua hiyo itawezesha kukuza biashara yao hususani kipindi hiki cha ushindani katika sekta ya usafirishaji wa anga.

“Tumejipanga kufanya safari mara tatu kwa wiki kwenye Hifadhi ya Taifa ya Serengeti,” alisema Rubani Maluli na kuongeza:

“Tumezoea kutumia viwanja vya lami, uwanja wa hapa hauna lami lakini upo vizuri kwanza una ukubwa wa kutosha kutua na kuruka. Lakini pia wapo askari wa wanyamapori wanaosaidia kufukuza wanyama endapo watakuwa wanaoingia uwanjani,”alisema Maluli

Naye muongoza watalii kutoka Kampuni ya Sense of Afrika, John Ngoma alisema kuanza kwa safari hizo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kunaweza kuwa kichochezo kikubwa cha wageni kutembelea hifadhi hiyo.

“Uamuzi huu ni mzuri sana kwani utakuza sekta hii ambapo kwa kuanzia tu umewezesha watalii 43 kutoka nchini Afrika Kusini kufika kwa wakati hifadhini humo na kuokoa fedha za kuunganisha ndege,” alisema Ngoma.


Mwisho. 

No comments:

Post a Comment