SERIKALI imeshauriwa kuacha
kuzunguka mlango wa nyuma kisha kukamata na kuwafungulia mashitaka baadhi ya viongozi
wanaosimamia maazimio ya kurejesha ardhi za umma na Taasisi za Serikali.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa juzi na Mbunge wa Jimbo la
Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari alipozungumza kwa niaba ya wabunge
wenzake.
Mkutano huo ulilenga kuwasilisha taarifa ya Mpango kabambe wa Mipango
miji kwa jiji hilo na viunga vyake mbele ya madiwani wa Halmashauri ya Jiji la
Arusha, Halmashauri ya wilaya ya Arusha na Meru.
Alisema viongozi wa kuchaguliwa na wananchi wanajitahidi
kusimamia maagizo ya Serikali ikiwamo ya kuhakikisha ardhi zinazomilikiwa
ofisi, Taasisi za Serikali hazivamiwa wala kuuzwa kwa watu binafsi.
“Tumepewa kura na wananchi, tunasimamia maazimio ya kuhakikisha ardhi
ya umma haivamiwi. Lakini wakati tukichukua uamuzi wa kulinda mali za umma
tunashangaa sisi ndio tunakamatwa kushitakiwa,” alisema Nassari na kuongeza:
“Tunakuomba Mkuu wa Mkoa tumekupa ushirikiano tunaahidi
kuendelea kukupa katika masuala kama haya, tukuombe msizunguke mlango wa nyuma
kutushitaki kwa kusimamia maagizo ya serikali,” alisema.
Nassari
alishitakiwa hivi karibuni na madiwani wote 29 wa Halmashauri ya Meru kwa madai
ya kuharibu uzio wa mfanyabiashara ambapo alisema kama wilaya ya Arumeru
isipopangwa sasa upo uwezekano wa kuwa na makazi ya hovyo zaidi huko baadaye.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha Daud Ntibenda aliyefungua
mkutano huo alisema, eneo la kuandaliwa kwa mpango kabambe linahusisha wilaya
za Arumeru, Arusha ambapo kwa upande wa wilaya ya Arusha inahusisha eneo lote
la Jiji.
Alisema ukubwa wa eneo hilo ni Kilometa za mraba 608 ambapo kati
ya hizo Kilometa 272 zipo katika Jiji la Arusha, Kilometa za Mraba 149 wilaya
ya Arusha, Kilimeta za mraba 187 Halmashauri ya wilaya ya Meru.
“Jiji la Arusha huwezi kulitenganisha na maeneo yaliyopo
Halmashauri mbili za Arusha na Meru kama vile Kisongo, Ngaramtoni, Tengeru na Usa
River. Ninaamini mango huu utakuwa ni Dira ya kusimamia na kuongoza Jiji hili
na viunga vyake kwa kipindi cha miaka 20 ijayo,” alisema Ntibenda.
Alisema kushirikishwa kwa madiwani hao waliochaguliwa Oktoba
2015 kumelenga kutoa nafassi ya ushiriki wao ili waweze kuona mawasiliano hayo
kwa mara ya kwanza na kutoa mapendekezo yao kabla ya kikao cha mwisho cha wadau
kitakachofanyika hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment