NA ELIYA MBONEA, ARUSHA
MWASISI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Mzee Edwin Mtei hivi karibuni katika mahojiano na Mtanzania nyumbani aliamua
kufunguka na kuonyesha furaha yake.
Furaha yake hiyo kama anavyosema mwenyewe ilikuwa imejificha
ndani ya moyo wake kwa takribani miaka 20 iliyopita tangu kulipoanzishwa Vyama vya Siasa vya upinzani
nchini mwaka 1992.
Katika mazungumzo yake pamoja na mambo mengine
aliyozungumzia anazungumzia pia safu mpya ya viongozi ndani ya CHADEMA, ambayo
imemfanya Mzee Mtei aliyewahi kuwa Gavana wa kwanza wa BOT kuonyesha furasa
yake.
Akifafanua kuhusu safu hiyo ya viongozi anasema, alipokuwa
kwenye uchaguzi huo Mliman City jijini Dar es Salaam, alikuwa na furaha kubwa
ya kuona kila walichokuwa wamekipinga miaka 20 iliyopita kikifanyika kama
walivyokusudia.
“Naweza kusema bila kigugumizi kabisa mimi ndiye Mzee
mwenye raha zaidi hapa nchini. Kwasababu kama leo hii unaweza kushuhudia vijana
wako wote wanavyojiimarisha katika uongozi hiyo ni sifa kubwa na njema kwa mzee
yeyote.
“Angalia jinsi tulivyofanya uchaguzi wa aina yake pale Dar
es Salaam. Tumepata viongozi vijana safi kabisa ile ni “Cream” ya uongozi ndani
ya CHADEMA itakayotuvusha kwenye uchaguzi Mwaka 2015.
“Cream ile ya viongozi nina uhakika kabisa wanaweza
kuongoza nchi hii kuelekea ukombozi wa taifa letu. Nina imani tutaokoka.
“Kwani tumejiandaa kuhakikisha kwamba ifikapo Oktoba 30,
Mwaka 2015 tutakuwa tumeiteka nchi hii na uhakika wa kuchukua madaraka tunao.
Sasa katika mazingira hayo kwanini nisiwe mzee mwenye raha kuliko wote nchini,”
anasema Mzee Mtei
Anasema kutokana na safu bora ya viongozi waliochaguliwa
ndani ya Chama, anayoimani kubwa kwamba Mwaka 2015 viongozi hao wakipelekwa
mstari wa mbele watakiongoza vyema chama kunyakua ushindi.
“Hawa tukiwapeleka mstari wa mbele hakika tutafika mbali,
na kwa sasa tunataka vijana wetu kila mmoja awe kwenye Kata yake ama Diwani au Mwenyekiti
katika Halmashauri, na baadaye waje kuwa wabunge,” anasema Mzee Mtei na
kuongeza:
“Nikiwa pale kwenye uchaguzi nilisema, Mimi ndio mzee
mwenye raha katika hii nchi kuliko wengine wote.” Maana yake ni kwamba hebu
angalia vijana wote ambao tulikuwa tunategemea walirudi na tukawachagua,”
anasema.
Mtei anawataja viongozi waliochaguliwa na kumfanya mwenye
furaha kuliko wazee wote, kuwa ni Katibu Mkuu wa CHADEMA Dk. Willbroad Slaa, Mwenyekiti
wa Taifa Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti Professa. Abdallah Safari, Naibu
Katibu Mkuu (Bara) John Mnyika, na Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar) Salum Mwalimu.
“Ukiwa na ‘cream’ kama hii ya uongozi hapo utagemea nini, huo ni ushindi tu. Hakika nilijiskia
raha sana, nikasema basi tu hakuna mzee mwenye raha kama mimi.
“Mambo haya tuliyaota wakati ule Mwaka 1992 tukiwa kwenye
baraza hili hapa nyumbani kwangu Tengeru mkoani Arusha leo yamefikia pazuri
kwani nashuhudia mambo yakifanyika kama tulivyopanga miaka 22 iliyopita,”
anasema Mzee Mtei.
Katika mtazamo wake wa CHADEMA imara Mzee Mtei aliyefanya
kazi katika nafasi tofauti kwenye serikali ya awamu ya kwanza ya Mwalimu
JuliusNyerere anasema, kama Hayati Baba wa Taifa angeendelea kuwa hai angekuwa
alishajiunga na Chama hicho.
Anazitaja sababu za Hayati Mwalimu kujiunga na Chama hicho
ilhali yeye ndiye alikuwa mwasisi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), anasema, tangu
alipoondoka madarakani Mwalimu alikuwa ameanza kuona ubora wa sera za CHADEMA.
“Mwalimu akiwa ameshaondoka madarakani, nakumbuka niliwahi
kumpelekea kitabu cha sera zetu, nilijkpeleka mwenyewe tukiwa nyumbani kwake
alikisoma vizuri sana. Tukiwa pale nyumbani kwake Msasani mwenyewe alisifu sana
Sera za CHADEMA.
“Na hata alipokwenda jijini Mbeya, Mwalimu alizungumzia
Chama chetu, na aliwaambia Watanzania CHADEMA ndio Chama kinachoweza kuwa na
sera ambazo zinaweza kuokoa nchi hii kutoka,”anasema Mzee Mtei.
Mzee Mtei anasema kwa mazingira ambayo tayari Hayati
Mwalimu Nyerere alikuwa amekwisha kuanza kuonyesha jinsi anavyovutiwa na sera
za CHADEMA ni wazi kwamba kama angeendelea kuwapo hadi leo basi angekuwa
alishajiunga na Chama hicho cha upinzani.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment