Wednesday, November 6, 2013

SERIKALI YAMKANA KATIBU MKUU WIZARA YA ELIMU PROF. MCHOME

SERIKALI imemkana Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome, na kudai taarifa aliyoitoa kuhusu mabadiliko ya madaraja ya ufaulu haikuwa ya Serikali.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi, alitoa kauli hiyo wakati akichangia hoja ya Mbunge wa Kawe Halima Mdee (CHADEMA), ambaye aliomba mwongozo wa Spika kutaka kujua hatua watakazochukuliwa mawaziri wa wizara hiyo kwa kulidanganya Bunge na umma.

Akitumia mwongozo wa kanuni ya 68 (7) sambamba na kanuni ya 63 (1) inayosomeka kuwa bila kuathiri masharti ya ibara 100 ya Katiba inayolinda na kuhifadhi uhuru na mawazo katika Bunge ni marufuku kabisa kuongea uongo bungeni,

Aliendelea kunuu kanuni hiyo na kusema mbunge yeyote anapokuwa amesema uongo bungeni ana wajibu wa kuhakikisha kwamba anatoa kauli au maelezo kuhusu jambo au suala ambalo yeye mwenyewe anaamini kuwa ni la kweli, na sio la kubuni au la kubahatisha.

Kutokana na kanuni hiyo Mdee alisema Naibu Waziri wa wizara hiyo Phillipo Mulugo juzi alilihadaa Bunge kwa kusema kuwa si kweli kwamba wizara imefuta kabisa divisheni 0 na kwamba vitu vinavyoandikwa kwenye magazeti na kwenye mitandao ya kijamii vinavyojadiliwa ni vya kizushi na si vya kweli, ilhali katibu wake alishatangaza.

Alisema nyaraka alizonazo ambazo Profesa Mchome alizitolea taarifa ya mabadiliko hayo zinaeleza kuwa wizara hiyo inafuta daraja 0 na kuweka daraja linalojulikana kama daraja la 5 ambalo litakuwa daraja la mwisho kabisa katika ufaulu.

“Naomba mwongozo wako Naibu Spika ni kweli kauli za mawaziri hazijadiliwi na ni kweli Spika alitoa agizo kuwa kauli ziletwe, kwa kuzingatia unyeti wa suala hili na kwa kuzingatia kwamba Naibu Waziri hakijui hata anachokisimamia, hudhani kwamba kuna haja ya hili suala likaletwa ili Bunge lako tukufu lijadili?”alihoji Mdee

Kauli ya Lukuvi

Lukuvi alisema “Ni kweli kwamba maelezo aliyoyatoa Mdee yalisemwa jana (juzi) na baadhi ya wabunge katika maswali ya nyongeza, nisema tu kwamba naibu waziri akisimama hapa ni kwa niaba ya serikali,

“Mfumo wa uendeshaji wa Serikali waziri ndiye mwendeshaji mkuu ikitokea katibu amesema jambo na waziri akatamka…., la waziri ndiyo la kuzingatia.

“Ukiona katibu anasema jambo fulani na waziri anatamka jambo jingine, la Serikali linakuwa la waziri,  kwa sababu hiyo sisi tunajiandaa kutekeleza agizo la Bunge ili kuleta maelezo ya kina na kuondoa mkanganyiko si kwa Mdee bali kwa Watanzania,”alisema Lukuvi.

Alisema kauli hiyo ya Serikali  itaondoa mkanganyiko juu ya maelezo yaliyotolewa na katibu mkuu na maelezo ya naibu waziri.

Naye Naibu Spika Job Ndugai, alitoa mwongozo ambapo alisisitiza kuwa kauli ya Serikali iwasilishwe bungeni haraka iwezekanavyo kwa sababu wanafunzi wa kidato cha nne wanafanya mtihani wa taifa na hawajui madaraja yakoje

“Ni kitu cha haraka kiletwe haraka sana na si kusubiri hata kidogo,”alisisitiza Ndugai.

Mwisho

No comments:

Post a Comment