Monday, March 4, 2013

MJUMBE BARAZA KUU UVCCM AFA KIFO TATANISHI



POLISI  Mkoani Arusha inawasaka wanawake wawili, wanaodaiwa kulala na mjumbe  wa  baraza kuu  la umoja wa vijana wa  (UVCCM) Taifa, kupitia Mkoa wa Arusha, Benson  Peter  Mollel (26) aliyefariki dunia ghafla juzi, katika chumba cha kulala wageni, Hotel ya Lush Garden, iliyopo barabara ya Jacaranda jijini Arusha.

Tukio hilo lilitokea Machi 3 mwaka huu, majira ya saa 7.00 mchana, baada ya mwili wa merehemu kugunduliwa na wahudumu wa hotel hiyo, walipotaka kukifanyia usafi chumba hicho alichokuwa amelala marehemu huyo .

Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Arusha, Liberatus  Sabas, alisema marehemu alifika hoteli hapo, Machi 2 mwaka huu, majira ya jioni na kupanga katika chumba namba 208, ambapo alilala hapo kwa siku mbili hadi mauti yalipo mkuta.

Alisema  hata hivyo Polisi baada ya kupata taarifa za tukio hilo, wanaendelea na msako mkali, kuwatafuta wanawake hao wanaodaiwa kuwa wawili, ambao walikuwa na marehemu kabla ya mauti ya ghafla kumfika, japo hadi sasa hakuna anayeshikiliwa.

Alisema kuwa mmoja wa wanawake hao alikwenda na marehemu hotelini hapo, majira ya saa 7.00 usiku, na mwingine alikwenda hotelini hapo asubuhi majira ya saa 5.00 asubuhi.

Aidha taarifa kutoka kwa wahudumu wa hoteli hiyo zimedai kwamba , marehemu aliwasili usiku, juzi Jumamosi hotelini hapo, akiongozana na mwanamke aliyetambulika kwa jina la Nancy na kuchukua chumba namba 208.

Taarifa hizo zimedai kwamba baada ya kuwa na mwanamke huyo walikaa kwa muda katika chumba hicho na baadaye walitoka pamoja na kurejea  usiku, wakiwa wote ambapo walilala pamoja hadi asubuhi.

Habari zaidi zimeeleza kuwa mwanamke huyo aliondoka na kumwacha marehemu akiwa amelala.

Hata hivyo ilipofika majira ya saa 5 asubuhi mwanamke mwingine, aliyetambulika kwa jina moja la Mariamu alifika katika hoteli hiyo na kuwaomba wahudumu wamwonyeshe chumba alichofikia marehemu.

Wakiwa katika majadiliano marehemu alipiga simu mapokezi na kuamuru wahudumu wa hoteli hiyo wampeleke  msichana huyo katika chumba alichofia marehemu  na kwamba ilipofika majira ya saa 6 mchana msichana huyo alionekana akitoka katika hoteli hiyo.

Baada ya msichana huyo wa pili kuondoka, wahudumu wa hoteli hiyo walijaribu kupiga simu katika chumba cha marehemu kwa lengo la kujua iwapo marehemu ataendelea kupanga katika chumba hicho ,hali kadhalika kukifanyia usafi.

Wahudumu hao walieleza kuwa simu katika chumba hicho ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa ndipo mmoja wa wahudumu huyo alipochukuwa jukumu la kwenda katika chumba hicho ili kujua iwapo bado kuna mtu ama ametoka.

Mhudumu huyo alifika katika chumba hicho na kukuta mlango upo wazi alijaribu kumwamsha marehemu kwa muda mrefu ikiwemo kumtingisha bila mafanikio na kuamua kutoa taarifa kwa uongozi wa hoteli hiyo ambao walifika na kubaini hali isiyoya kawaida.

Uongozi wa hoteli hiyo ulitoa taarifa polisi na polisi baada ya kufika waliuchukua mwili  wa marehemu na kwenda kuuhifadhi katika hospitali ya mount meru kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu.

Kamanda wa polisi mkoani Arusha alisema uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea na kwamba hakuna anayeshikiliwa juu ya tukio hilo.

Hata hivyo kumekuwepo na taarifa za kutatanisha juu ya tukio hilo huku taarifa za awali zikihusisha tukio hilo na visa vya kisiasa ,huku taarifa zingine pia zikidai  tukio hilo linahusiana na masuala ya ugomvi wa kibiashara kwani kabla ya tukio hilo marehemu alikuwa akifanya biashara ya madini.

Pia taarifa zingine zinadai kuwa marehemu huenda alitumia dawa za kuongeza nguvu za kiume kwa lengo la kuwaridhisha wanawake hao ambao walikuja kwa nyakati tofauti kwa lengo la kustarehe na marehemu .

Taarifa za mazishi ya kiongozi huyo chipukizi wa chama bado hazijafahamika japo vikao vya chama na familia vinaendelea kwa siri .

Mwisho.

No comments:

Post a Comment