Thursday, January 31, 2013

WANANCHI KUNUFAIKA NA SH. BILIONI 1.6 ZA WATALII WA MIAMVULI




WANANCHI waishio pembezoni na maeneo jirani na Mlima Kilimanjaro watarajia kunufaika na ziara ya watalii marubani 100 wa miamvuli maalumu wanaopanda Mlima huo ambapo watachangisha Dola za Marekani Milioni 1 sawa na Sh. Bilioni 1.6.

Kwa sasa Dola Moja ya Marekani kwenye maduka ya kubadilishia fedha jijini Arusha imefikia kiasi cha Sh. 1,650.  

Watalii hao zaidi ya 100 wanaanza kupanda Mlima Kilimanjaro kesho na itawachukua siku 7 kufika kilelele cha Uhuru Peark ambapo baada ya hapo wataanza kushuka kwa kutumia miamvuli hiyo ikiwa ni huduma mpya katika sekta ya utalii nchini kufanywa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mbele ya watalii hao kutoka mataifa 25 duniani, Meneja wa Uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa nchini (TANAPA), Paschal Shelutete alisema, ziara hiyo inatarajiwa kuchangisha kiasi cha Dola za Marekani Milioni 1.

Shelutete alisema fedha zitakazokusanywa katika ziara hiyo zimepangiwa kuhudumia jamii mbalimbali nchini zinazozunguka maeneo ya Mlima Kilimanjaro na maeneo jirani.

Alisema fedha hizo zitapitishwa katika Taasisi tatu za “One Foundation inayojishughulisha na kampeni dhidi ya Ukimwi, Plan with a Purpose na World Serve International” kwa ajili ya kuzifikisha kwa jamii na maeneo husika.

“Fedha zitatumika kuchimba visima, zitaingizwa kwenye kampeni za Ukimwi, matatizo ya maji. Lakini pia ziara hii itatoa nafasi za ajira za kwa vijana takribani 650 watakaokuwa wakisaidia wageni,” alisema Shelutete.

Aliendelea kufafanua kwamba watalii hao pindi watakapofika kilele cha Mlima Kilimanjaro, Uhuru Peark Februari 5, Mwaka huu ndio wataanza safari ya kushuka hewani kwa kutumia miamvuli hiyo.

“Tayari maandalizi yote yameshakamilika ikiwa ni pamoja na maeneo ya kutua ambapo watashukia Shule ya Msingi Umbwe na Kibosho Chuo cha Ufundi 

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Maji Tech Lewis Kopwe akizungumzia fedha hizo alisema tayari wameshalitenga eneo la Simanjiro mkoani Manyara ambako watachimba visima vya maji safi, kisha kujenga vyumba vya madarasa.

Alisema zaidi ya watu 16,000 wanatarajiwa kunufaika na msaada huo utakaoelekezwa katika eneo la wilaya ya Simanjiro kupitia ziara hiyo ya watalii. 

Naye Mkurugenzi wa Top of Africa Silvano Mvungi ambaye ni muongoza watalii hao alisema kwamba mazingira ya zaiara hiyo yamekwisha kuandaliwa  

Mwisho.
 

No comments:

Post a Comment