*Apandishwa kizimbani, akosa dhamana
apelekwa gerezani
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) mkoani Arusha imempandisha kizimbani Mwandishi wa habari wa kujitegemea
Joseph Ngilisho kwa tuhuma za kuomba rushwa ya Sh. Milioni 2.
Mwendesha Mashitaka wa TAKUKURU
Rehema Mteta alidai juzi mbele ya Hakimu Mkazi Hawa Mguruta wa Mahakama ya
Arusha kuwa Ngilisho anatuhumiwa na makosa matatu, kuomba, kushawishi na kupokea
Sh. 500,000 kati ya Sh. Milini 2 alizoomba.
Mteta alida kwamba mtuhumiwa huyo
anadaiwa kutenda makosa hayo katika siku tofauti akiwa jijini Arusha.
Mwendesha Mashitaka Mteta alifafanua
kwamba Januari 12, Mwaka huu, Ngilisho anadaiwa kuomba Sh. Milioni 2 kutoka
Ofisa Mwandamizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Phil Kleruu ili asiandike
vibaya habari zake ndani ya Gazeti la Dira.
“Shitaka la pili anadaiwa kulitenda
Januari 25 Mwaka huu, ambapo aliomba rushwa kutoka kwa ofisa huyo ili aandike
habari za kumsafisha gazetini.
“Januari 28, Mwaka huu, mtuhumiwa
alikamatwa akipokea Sh. 500,000 ikiwa ni sehemu ya malipo ya Sh. Milioni 2
alizoomba,” alisema Mteta.
Kwa upande wake akitakiwa
kuthibitisha madai hayo mshitakiwa Ngilisho anayewakilishwa na Wakili
Edmund Ngelemi, alipinga madai hayo.
Akitoa nafasi ya dhamana kwa
mtuhumiwa Hakimu Mguruta alisema mshitakiwa anatakiwa kuwa na wadhamini watatu
huku mmoja kati yao akiwa ni mtumishi wa serikali.
Pamoja na kupatikana kwa wadhamini
hao bado Hakimu alikataa nyaraka zao kwa madai zilikuwa hazijajitosheleza
kisheria,hatua iliyomsababishia mtuhumiwa kupelekwa mahabusu katika gereza la
Kisongo hadi hapo taarifa zitakapokuwa zimekamilika
Kesi hiyo imeahirishwa hadi
Februari 12, Mwaka huu itakapotajwa tena.
Habari kutoka eneo la tukio
alikokamatwa mwandishi huyo zilidai kwamba mara baada ya kupokea fedha hizo
aliwashtukia maofisa wa TAKUKURU wakimzunguka ndipo alikimbia.
Habari hizo ziliendelea kubainisha
kuwa mbio za mwandishi huyo hazikufua dafu kutokana na kukimbia kuliko
sababisha kuchana suruali yake, na kujikuta akiingia akiingia ndani ya ofisi za
Usalama wa Taifa zilizopo jirani na Hoteli ya East Africa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment