Na ELIYA MBONEA
-UHURU PEAK
WATANZANIA 19 wakiwamo Wanahabari, askari wa Jeshi la Wananchi
(JWTZ) na maofisa wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) wamefika kilele cha
Mlima Kilimanjaro (Uhuru Peak ) ikiwa ni maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa
Tanganyika Desemba 9, Mwaka huu.
Msafara huo wa watu 35 ulianza safari Desemba 5, Mwaka huu
ukipitia Marangu chini ya Mkuu wa Majeshi na Mwenyekiti wa Bodi ya TANAPA
Jenerali Mstaafu George Waitara pamoja na Mkuu wa Oparesheni na Mafunzo Makao
Makuu ya Jeshi la Nchi Kavu, Brigedia Jenerali Jairos Mwaseba.
Akizungumza na wanahabari na maofisa wa JWTZ katika kilele cha
Uhuru Peak Futi 5,895 kutoka usawa wa bahari, Meneja Uhusiano wa TANAPA Paschal
Shelutete alisema, mbali na maadhimisho ya miaka 55 ya uhuru ziara hiyo
ililenga pia kuhamasisha utalii wa ndani kwa Watanzania.
Shelutete aliyekuwa miongozi mwa waliofika kileleni alisema,
vivutio kama Mlima Kilimanjaro na vingine walivyopewa Watanzania zawadi
na Mwenyezi Mungu wanapaswa kujiona fahari mbele za mataifa mengine kwa kuwa na
vivutio vizuri vya utalii.
“Watanzania wanapaswa kuwa na fahari na maeneo ya vivutio vya
utalii walivyopewa na Mungu. Ni wahamashe wananchi wenzangu wajipange katika
maisha yao kutimiza ndoto ya kupanda mlima mrefu kuliko yote Afrika,” alisema
Shelutete na kuongeza:
“Kwa kushirikiana na JWTZ na Kampuni ya Utalii ya Zara tuliandaa
ziara ya kupanda Mlima Kilimanjaro na kuhahakikisha siku ya kilele cha Uhuru
nasi tunakuwa kilele cha Uhuru Peak.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi Jeneral Mstaafu Waitara akizungumza
wakati wa halfa ya kuwapokea wapanda mlima hao pamoja na mambo mengine
aliwataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuutangaza mlima huo pamoja na
vivutio vingine.
“Nimefarijika sana kuona waandishi wa habari Saba wakiwa
wamefanikiwa kufika vituo tofauti lakini zaidi kwa watano waliofika Uhuru Peak.
“Pongezi maalum kwa wote 15 waliojitokeza, kwa waliofika mpaka
mwisho wanamajibu mazuri. Na hii ninyi waandishi mliopanda mmetoa changamoto
kwa waandishi wenzenu kuja kupanda Mlima Kilimanjaro,” alisema Jenerali Mstaafu
Waitara.
Baada ya kujionea mazingira ya maeneo ya kuelekea kileleni
Jenerali Mstaafu Waitara aliishauri TANAPA kufanya maboresho kwenye vituo vya
kulala na kupumzikia wageni wanaopanda mlimani.
“Nimeingia kwenye vyumba kuna mambo tunapaswa kuyafanyia
marekebisho kidogo ili kuongeza ushawishi kwa watu wengine ikiwamo kada ya
viongozi na watu mashuri.
“Kwamba tuwe angalau na vyumba vinavyojitegemea kwa kila kitu
badala ya sasa hivi mgeni analazimikakulala na kutoka nje kwa ajili ya mahitaji
mengine.
“Pengine viongozi wanaweza kuwa wanasita kuja kupanda mlima kwa
sababu tu ya vitu vidogo, hebu tujaribu kuboresha ili tushawishi watu mashuhuri
waje,” alisema Jenerali Mstaafu Waitara.
Mbali na askari wa JWTZ, waandishi wa habari waliofika kilele
cha Uhuru Peak ni pamoja na Dikson Busagaga (Tanzania Daima), Eliya Mbonea
(Mtanzania), Ramadhan (Mvungi Star Tv),Charles Ndagula (Tanzania Daima) na
Shelutete kutoka TANAPA.
Waandishi wa habari waliofanikiwa kufika kituo ha Stela chenye
futi 5,756 ni Iddi Uwesu (Azam Tv) na Ramadhan Siwayombe (Tanzania Daima)
Mwisho.
No comments:
Post a Comment