Monday, February 4, 2013

MBUNGE JAMES MBATIA AHOFIA HOJA YAKE KUCHAKACHULIWA

MBUNGE wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR Mageuzi), amesema Serikali imejiandaa kuchakachua mtaala wa elimu inaotarajia kuuwasilisha bungeni Februari 6 mwaka huu.

Pia amesema, anao ushahidi kwamba kuna kikundi cha watu wachache wamejifungia huko Dar es Salaam wanataka kubadilisha muhtasari uliopo na kuugeuza kuwa ndio mtaala.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR mageuzi, alisema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa tangu Oktoba 30 mwaka jana, alishindwa kuwasilisha bungeni kile kinachoitwa mtaala badala yake alipiga chenga hadi wiki iliyopita.

Alisema, ni suala la kutia shaka tangu mwaka jana alipoomba kupewa mtaala huo hadi leo, lakini waziri bado anaomba aongezewe siku kana kwamba anakwenda kuuagiza nje ya nchi.

“Wakae wakijua, mtaala wa elimu ni mmoja, na haupaswi kuwa siri, hawawezi kukaa kikundi cha watu sita au saba wakasema wanaandaa mtaala kinyemela.

“Nasisitiza hatujawahi kuwa na mtaala rasmi Tanzania tangu mwaka 1961, huko walikokaa na kujifungia ili waje na mtaala wa kuchakachua hatutaukubali, tunajua wanataka kutuletea rasmu iliyopo kwamba ndiyo mtaala, ninaitahadhalisha serikali iache kabisa mchezo huo mchafu watawaaibika.

Huku akionyesha nakala ya rasimu hiyo, alisema, Waziri Dk. Kawambwa alilieleza Bunge kwamba mtaala unaotumika niwa  2005 huku rasmu ikionyesha chapa ya kwanza kwa shule za msingi hadi vyuo vya ualimu ikiwa niya mwaka 2012

“Rasmu ya shule za awali mpaka vyuo vya ualimu iliyoandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania mwaka 2010, na chapa ya kwanza 2012, sasa inawezekanaje chapa hiyo itoke 2012 wakati tunaambiwa mitaala inayotumika sasa niya 2005? Alihoji na kuendelea.

“Unajua kinachompa hofu ni hii chapa ya mwaka 2012, mitaala yote ya elimu ya awali, msingi, sekondari, sekondari kidato cha tano na sita na vyuo vya ualimu rasmu zote zimechapwa mwaka 2012.

“Sasa waziri atueleze, kwa nini mtaala wa mwaka 2005 uchapwe mwaka 2012? Hiyo ndiyo hofu yao” alisema Mbatia. 

“Hali ni tete, tunao ushahidi wa kutosha na ni mwingi, unapofanya ufisadi kwenye elimu ni kuliangamiza taifa, wanaleta mgongano kwenye kanuni ili kulinda uovu.

Naibu Spika mliona alivyomlinda moja kwa moja waziri, hoja yangu imetengenezwa na kupitiwa na wataalamu wa Ofisi ya Spika, sasa iweje tena waanze kuipindishana kuitafutia sababu zisizokuwa za msingi.

 “Nawaomba Watanzania wasikubali maisha yao yachezewe namna hiyo,na mimi nawaambia bado sijahitimisha hoja yangu” alisema.

Alisema, serikali inataka kuleta mkanganyiko usiokuwa na maana kwa sababu kiutaratibu, kinachoanza kuandaliwa katika masuala ya elimu ni sera, ikifuatiwa na mtaala na mwisho rasmu au muhtasari.

Ambapo alisema, sera yenyewe ya elimu ndiyo kwanza ipo katika mchakato wa kuandaliwa, sasa anahoji mtaala huo utatoka wapi.

No comments:

Post a Comment